Mahakama yawaagiza madaktari wanaogoma kurudi kazini Kenya

Image caption Madaktari wanataka nyongeza ya mishahara ya asilimia 300

Mahakama ya kutatua mizozo ya wafanyakazi nchini Kenya, imetangaza mgomo wa madaktari unaoendelea nchini humo kuwa ulio kinyume cha sheria na kuwataka warejee kazini mara moja.

Mgomo huo ulioanza zaidi ya wiki moja iliyopita, umekwamisha huduma za matibabu kwenye hospitali za umma kote nchini na unaaminiwa kuwa chanzo cha vifo vya takriban watu 20.

Watoa huma za afya wa kibinafsi pia nao wanatarajiwa kujiunga na mgomo huo kuonyesha uzalendo kwa wenzao walio kwenye hospitali za umma.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mgomo huo umeathiri pakubwa huduma za afya nchini Kenya

Wanataka nyongeza ya mshahara ya asilimia 300 kwa madaktari na kati ya asilimia 25 na 40 kwa wauguzi, ikiwa ni sehemu ya makubaliano waliyotia sahihi na serikali mwaka 2013.

Chama cha madaktari nchini Kenya kimekataa pendekezo walilopewa na serikali kwa madaktari walio na mishahara ya chini.

Rais Uhuru Kenyatta pia naye amewashauri madaktari hao kurudi kazini.