Duterte akiri kuua watu mwenyewe Ufilipino

Duterte bado anapendwa sana na watu Ufilipino Haki miliki ya picha AFP
Image caption Duterte bado anapendwa sana na watu Ufilipino

Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte amekiri kwamba aliwahi kuua washukiwa wa uhalifu mwenyewe alipokuwa meya wa Davao.

Alikuwa meya wa mji huo wa kusini mwa Ufilipino kwa miongo miwili, ambapo alijizolea sifa kwa kupunguza visa vya uhalifu.

Hata hivyo, amekosolewa kwa kuunga mkono magenge ya wauaji.

Bw Duterte alikuwa akihutubu katika mkutano wa viongozi wa kibiashara Ufilipino mnamo Jumatatu kabla ya kufunga safari kuelekea ng'ambo.

Maneno hayo ndiyo ya karibuni zaidi kutolewa na Duterte ambayo yamezua utata.

"Nilipokuwa Davao binafsi nilikuwa nafanya hivyo. Ili kuwanonyesha jamaa hao (polisi) kwamba iwapo ninaweza kufanya hili, nanyi pia basi mnaweza," alisema.

"Na ningezunguka Davao kwa pikipiki, nikiwa na pikipiki kubwa, na kuzunguka barabara za mji, nikitafuta wahalifu. Nilikuwa natafuta makabiliano ndipo nipate fursa ya kuua."

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Duterte alitoa hotuba hiyo kabla ya kuondoka kuelekea Cambodia na Singapore

Matamshi hayo yanakaribiana na matamshi aliyoyatoa mwaka 2015, alipokiri kuua wanaume watatu walioshukiwa kutekeleza makosa ya utekaji nyara na ubakaji mjini Davao.

Lakini saa chache kabla ya kusema hayo, alikuwa amesisitiza kwamba "Mimi si muuaji", alipokuwa akitoa hotuba wakati wa tuzo ya mtu aliyefanya vyema zaidi Ufilipino.

Karibu watu 6,000 wanadaiwa kuuawa na polisi na magenge ya watu wenye silaha tangu Duterte aanzishe vita dhidi ya mihadarati baada ya kuchaguliwa mwezi Mei.

Amesema hawezi kuomba radhi kuhusu sera hiyo.

Wakati mmoja, alisema: "Hitler aliwaua Wayahudi milioni tatu ... Kuna waraibu milioni tatu wa mihadarati. Ninaweza kufurahia sana kuwaua."

Mwandishi wa BBC Jonathan Head anasema Bw Duterte amekuwa mara kwa mara akisema hajali kuhusu haki za kibinadamu na amedokeza kwamba mawakili wanaotetea washukiwa wanaoandamwa kwenye kampeni yake ya kuua walanguzi wa dawa huenda pia wakaandamwa.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii