Polisi wapya Uingereza kuhitajika kuwa na digrii

Makurutu wa polisi

Makurutu wapya wanaotaka kujiunga na idara ya polisi England na Wales watahitajika kuwa na shahada ya kwanza kuanzia 2020, Chuo cha Polisi kimetangaza.

Hatua hiyo inatarajiwa kusaidia kikosi cha polisi kukabiliana na aina mpya za uhalifu.

Maafisa wanaotaka kujiunga na kikosi cha polisi wanaweza kupokea mafunzo ya digrii wakiwa wanafanya kazi kwa miaka mitatu, wasomee masomo ya baada ya shahada ya kwanza au wawe wamesomea shahada ya kwanza moja kwa moja.

Baraza Kuu ya Taifa la Polisi nchini Uingereza limesema mabadiliko hayo mapya yatawezesha kuboresha kikosi hicho na kukifanya kutembea na majira.

Kwa sasa, masharti ya kujiunga na vikosi mbalimbali vya polisi Uingereza huwa tofauti.

Baadhi huhitaji makurutu wawe wamemaliza masomo ya upili au wawe na cheti katika huduma za polisi. Kuna vikosi vingine hutaka makurutu angalau wawe na uzoefu kiasi katika kutekeleza majukumu yanayolingana na ya polisi.

Chuo cha Polisi kimesema kwa sasa ni theluthi moja peke (38%) ya wanaojiunga na vikosi vya polisi ambao wana elimu ya kuanzia shahada ya kwanza kwenda juu.

Chuo hicho kinafanya mashauriano na vyuo vikuu 12 viwe vikitoa kozi za huduma za polisi.

Mada zinazohusiana