Baraza jipya la mawaziri latangazwa DR Congo muhula wa Kabila ukimalizika

Rais Kabila ameongoza tangu mwaka 2001 Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Rais Kabila ameongoza tangu mwaka 2001

Makabiliano kati ya waandamanaji wanaopinga kuendelea kusalia madarakani kwa Rais Joseph Kabila nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na maafisa wa polisi yalishuhudiwa usiku katika mji mkuu Kinshasa na miji mingine.

Milio ya risasi ilisikika kaskazini mwa mji huo mkuu.

Muhula wa rais Kabila kikatiba ulifikia kikomo saa sita usiku wa kuamkia leo, lakini uchaguzi wa urais haukufanyika Novemba na hivyo basi hakuna mtu wa kumrithi.

Muda mfupi baada ya muhula wake kumalizika, waziri mkuu Samy Badibanga kupitia televisheni alitangaza kuundwa kwa serikali mpya ambayo inajumuisha viongozi kadha wa upinzani.

Vyama vikuu vya upinzani vilitangaza kwamba vitapinga juhudi zozote za kujaribu kuongeza muda wa Rais Kabila madarakani.

Mazungumzo ambayo yamekuwa yakiongozwa na maaskofu wa kanisa Katoliki kutafuta suluhu ya mzozo huo yanatarajiwa kurejelewa Jumatano.

Baraza la mawaziri lililotangazwa na Bw Badibanga Jumatatu lina mawaziri na mawaziri wasaidizi 67.

Kuna manaibu watatu wa waziri mkuu, mawaziri 34 wa wizara, mawaziri saba wa dola na manaibu waziri 23.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Maandamano ya kumtaka kabila kuondoka madarakani yafanyika duniani

Baadhi ya mawaziri waliokuwa wanahudumu wamefutwa kazi na nafasi 20 mpya kuundwa, na kuongeza idadi kutoka 47 hadi 67.

Mmoja wa manaibu wa waziri mkuu ni seneta She Okitundu, ambaye atasimamia masuala ya mambo ya nje ya utangamano wa kikanda.

Emmanuel Ramazani Shadari ameteuliwa waziri wa ammbo ya ndani naye Jose Makila akateuliwa waziri wa uchukuzi na mawasiliano.

Makamu wa rais wa zamani Azarias Ruberwa ameteuliwa waziri wa serikali anayehusika na ugatuzi na mageuzi ya kitaasisi.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii