Mkenya ashinda taji la malkia wa urembo Afrika

Malkia wa urembo kutoka Kenya Eveylyn Njambi katika shindano la malkia wa urembo duniani 2016 nchini Marekani Haki miliki ya picha ZACH GIBSON
Image caption Malkia wa urembo kutoka Kenya Eveylyn Njambi katika shindano la malkia wa urembo duniani 2016 nchini Marekani

Malkia wa Urembo kutoka Kenya Evelyn Njambi Thungu aliibuka miongoni mwa warembo watano bora katika mashindano ya malkia wa urembo duniani 2016 yaliofanyika nchini Marekani.

Njambi ambaye sasa ndio malkia mrembo barani Afrika sasa anajiunga na Kevin Owiti pia kutoka Kenya ambaye alishinda taji la Mr. Afrika.

Njambi alichukua mahala pake Roshanara Ebrahim ambaye aliondolewa kwa kukiuka maadili ya shindano hilo.Njambi alikuwa wa pili katika shindano la Miss World Kenya 2016.

Miss World Kenya apokonywa taji lake

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 23 ambaye ni mwanafunzi wa somo la mapambo ya nyumba katika chuo kikuu cha Maseno ndiye mshindi wa tuzo la Malkia mrembo kutoka kaunti ya Kiambu 2016.

Wakati alipokuwa mshindi wa tuzo la Miss Kiambu alishiriki katika maswala mbali mbali ya kaunti yake ikiwemo kuwasaidia watoto kwenda shule.

Haki miliki ya picha ZACH GIBSON
Image caption Evelyn Njambi kutoka Kenya punde tu alipoorodheshwa miongoni mwa Malkia watano bora duniani

Malikia wa urembo kutoka taifa la Puerto Rico Stephanie Del Valle ndiye aliyeibuka mshindi wa mashindano hayo siku ya jumapili na kushinda zawadi kuu.

Del Valle mwenye umri wa miaka 19 ambaye ni mwanafunzi wa somo la sheria na mawasiliano alisema kuwa ni heshima na jukumu kubwa kuwakilisha taifa lake.

Aliyechukua nafasi ya pili alikuwa Yaritz Miguelina Reyes Ramirez kutoka Jamhuri ya Dominican aliyefuatwa na Natasha Mannuela kutoka Indonesia.

Malkia mwengine aliyeorodheshwa katika malkia watano bora ni Catriona Elisa Gray kutoka Ufilipino.

Zaidi ya mataifa 100 yaliwakilishwa katika shindano hilo lililofanyika katika ukumbi wa kitaifa wa National Harbor karibu na mji wa Washington DC.