Maficho ya Boko haram kuwa kambi ya jeshi Nigeria

Msitu wa sambisa kubadilishwa na kuwa kambi ya jeshi la Nigeria
Image caption Msitu wa sambisa kubadilishwa na kuwa kambi ya jeshi la Nigeria

Kiongozi mkuu wa jeshi la Nigeria anasema kwamba, msitu mkubwa wa Sambisa uliokuwa makao makuu ya kundi la wapiganaji wa Boko Haram, utabadilishwa na kuwa kituo cha mafunzo ya kijeshi.

Jenerali Luteni Tukur Buratai, amesema kuwa hiyo itazuia kuchipuka tena kwa Boko Haram na kuchukua udhibiti wa eneo hilo.

Jeshi la Nigeria, limesema kuwa limesambaratisha kabisa eneo la mwisho la kundi hilo katika msitu huo wa Sambisa siku ya Ijumaa.

Inaaminika kuwa wanamgambo wa Boko Haram walikimbilia maeneo yaliyo karibu na mpaka na mataifa ya Chad na Niger, muda mfupi kabla ya kambi hiyo kuvamiwa.

Wapiganaji hao waliamua kufanya msitu wa Sambisa kuwa ngome yao kuu, baada ya kupoteza udhibiti wa miji kadhaa kaskazini mashariki mwa Nigeria miaka miwili iliyopita.