Pakistan: Pombe haramu yawauwa watu 20 katika mkesha wa Krismasi

Waombolezaji mjini Punjab Haki miliki ya picha AP
Image caption Jamaa wa mmoja wa watu waliokufa wakiomboleza baada ya marehemu kunywa pombe haramu wakati wa sherehe za Krismasi

Polisi nchini Pakistan wanasema takriban watu ishirini na sita wamekufa baada ya kunywa pombe haramu usiku wa kuamkia Krismas.

Afisa wa polisi katika eneo hilo Muhammad Nadeem amesema kuwa kundi la watu katika mji wa Toba Tek uliopo kilomita zaidi ya 330 kusini mwa mji mkuu, Islamabad walitengeneza kileo haramu mkesha wa Krismasi na kukinywa.

Amesema kuwa kumi na tisa miongoni mwa waliokufa walikuwa ni wakristo na wawili walikuwa ni waislam.

Baadhi ya ripoti zinasema kuwa wengine zaidi ya mia moja waliokunywa pombe hiyo wanapata matibabu hospitalini.

Kutokana na kwamba uuzaji wa pombe unadhibitiwa sana nchini Pakistan, pombe za bei ya chini zenye sumu zimekuwa zikitengenezwa majumbani mwa watu.

Ni tukio la hivi karibuni na vifo vilivyosababishwa na pombe yenye sumu nchini Pakistan baada ya watu wengine 11 kufa mwezi Oktoba, pia katika jimbo la Punjab.

Mohammad Nadeem amemueleza mwandishi wa BBC idhaa ya Urdu kwamba watu 40 wamelazwa katika hospitali za Toba Tek Singh na Faisalabad ili kusafisha tumbo zao.

"Wanaume hao wallikunywa pombe hiyo usiku tarehe 25 Disemba na kwenda nyumbani. Maafa yalianza asubuhi yake ambapo walishindwa kunyanyuka kutoka vitandani mwao huku wengine wakijihisi kuwa na maumivu makali ," alisema Nadeem.

.