Urusi: Tutalipiza kisasi

Msemaji wa rais Vladmir Putin amesema kuwa hatua zitakazochukuliwa na Urusi zitaiathiri Marekani.
Image caption Msemaji wa rais Vladmir Putin amesema kuwa hatua zitakazochukuliwa na Urusi zitaiathiri Marekani.

Urusi imeonya kwamba italipiza kisasi hatua ya rais wa Marekani Barrack Obama ya kuwatimua wanadiplomaisa thelathini na tano wa Urusi kufuatia tuhuma kwamba Urusi iliingilia maswala ya uchaguzi wa Marekani kwa njia ya udukuzi wa mitandaoni.

Obama amesema Urusi pia imekuwa ikiwadhalilisha maafisa wa Marekani.

Kwa upande wake, rais mteule Donald Trump ambae mara kwa mara amekuwa akizipuuzilia taarifa hizo za udukuzi, sasa amesema atakutana na wakuu wa kiintellijensia wa Marekani ili kupata undani zaidi wa swala hilo.

Msemaji wa rais Vladmir Putin amesema kuwa hatua zitakazochukuliwa na Urusi zitaiathiri Marekani.

Hatahivyo amesema kuwa Urusi itasubiri hadi rais mteule Donald Trump ambaye amepinga tuhuma hizo za udukuzi atakapochukua mamlaka.

Urusi imekana madai yoyote ya udukuzi na kuvitaja vikwazo hivyo vya Marekani kama visivyo na msingi.

Siku ya Alhamisi, Idara ya maswala ya kigeni nchini Marekani ilitangaza kwamba mabalozi hao 35 kutoka Urusi pamoja na wasaidizi wao huko San Fransisco kuwa watu wasiotakiwa Marekani na kuwapatia wao na familia zao muda wa saa 72 kuondoka nchi humo.