Rais wa Korea Kusini akataa kwenda mahakamani

Rais Park Geun hye wa Korea Kusini alikataa kuhudhuria kusikilizwa kwa kesi yake ya ufisadi Haki miliki ya picha Reuters/Yonhap
Image caption Rais Park Geun hye wa Korea Kusini alikataa kuhudhuria kusikilizwa kwa kesi yake ya ufisadi

Mahakama ya kikatiba nchini Korea Kusini imesikiza kwa muda mfupi kesi ya kushtakiwa kwa rais Park Geun hye ambayo kiongozi huyo anayepigwa vita hakuudhuria.

Kikao hicho kilifungwa baada ya dakika tisa na kuahirishwa hadi siku ya Alhamisi kutokana na kutokuwepo kwa bi Park.

Wabunge walipiga kura ya kumshtaki bi Park mwezi uliopita kutokana na kashfa ya ufisadi.

Mwandani wake wa karibu Choi Soon-sil ameshtakiwa na utumizi mbaya wa madaraka.

Bi Park anadaiwa kuhusika ,swala analopinga.

Kesi hiyo ya rais Park inasikizwa katika mahakama hiyo na majaji tisa.

Majaji hao wana siku 180 kuamua iwapo bi Park ambaye amesimamishwa kazi anafaa kuendelea na kazi ama kuondoka mamlakani.

Ijapokuwa mahakama hiyo imetaka awepo wakati kesi yake inapoendelea, amesema hatohudhuria hadi pale kutakapokuwa na swala maalum, kulingana na shirika la habari la Yonhap.

Iwapo bi Park atakosa kuwasili mahakamani kwa mara ya pili, kesi hiyo inaweza kuendelea bila yeye.

Majaji hao watachunguza iwapo bi Park alitumia vibaya madaraka, alihusika katika kuchukua hongo na iwapo alikiuka sheria miongoni mwa maswala mengine.