Gambia: Mkuu wa uchaguzi Momar Njai aenda mafichoni

Alieu Momar Njai alisimamia uchaguzi ambao Yahya Jammeh alishindwa Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Alieu Momar Njai alisimamia uchaguzi ambao Yahya Jammeh alishindwa

Mkuu wa tume ya taifa ya uchaguzi nchini Gambia ameenda mafichoni, familia yake imeambia BBC.

Alieu Momar Njai, aliyetangazwa kwamba Rais Yahya Jammeh alikuwa ameshindwa uchaguzini mwezi jana, ametoroka nchi hiyo kwa mujibu wa mwanawe Momodou.

Rais Jammeh awali alikubali kushindwa, lakini baadaye akabadili msimamo wake na kukataa kung'atuka.

Maafisa wa usalama walitwaa udhibiti wa makao makuu ya tume ya uchaguzi baadaye.

Akiandika kwenye Facebook Jumanne jioni, Momodou Alieu Njai alisema babake yuko salama na akawashukuru watu kwa maombi yao.

Rais Jammeh, ambaye ameongoza Gambia kwa miaka 22, alishindwa na Adama Barrow katika uchaguzi uliofanyika 1 Desemba kwa mujibu wa tume ya uchaguzi.

Bw Barrow alipata asilimia 45 ya kura.

Vituo vitatu vya redio vya kibinafsi vimefungwa na serikali tangu Jumapili.

Juhudi za wanadiplomasia kumshawishi Bw Jammeh kukubali kung'atuka madarakani kufikia sasa hazijafua dafu.

Muungano wa kiuchumi wa nchi za Afrika Magharibi, Ecowas, umetishia kuwekea Bw Jammeh vikwazo asipoondoka madarakani.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii