Antonio Conte: Tottenham inaweza kushinda ligi

Antonio Conte wa Chelsea asema Tottenhama inaweza kuwania taji la ligi Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Antonio Conte wa Chelsea asema Tottenhama inaweza kuwania taji la ligi

Mkufunzi wa klabu ya Chelsea Antonio Conte anasema kuwa Tottenham inaweza kushinda taji la ligi kuu ya Uingereza baada ya kusitisha ushindi wa mechi 13 mfululizo wa Chelsea kwa kuichapa 2-0 katika uwanja wa White Hart Lane.

Vichwa viwili vilivyopigwa na Dele Ali viliisaidia Tottenham kuishinda Chelsea tangu mwezi Septemba na kuiwacha Spurs ikiwa pointi saba nyuma ya viongozi hao katika nafasi ya tatu.

''Tottenham ni timu nzuri sana na kwa kweli ni mojawapo ya timu ambazo zinaweza kuwania taji la ligi'', alisema Conte.

Mkufunzi Mauricio Pochettino alisema kuwa Spurs inaweza kupigania vitu vikubwa.

Tottenham ndio waliokuwa wapinzani wakuu wa Leicester katika kipindi kirefu cha msimu uliopita huku ikiwa nyuma kwa pointi 5 zikiwa zimesalia mechi nne, lakini ikamaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya Arsenal baada ya kupata matokeo mabaya.

Msimu huu hawajafungwa nyumbani katika ligi na Pochettino ,mwenye umri wa miaka 44 anasema kuwa matokeo mazuri ndio yatakayosaidia kupanda katika kilele cha ligi.