Urusi kupunguza wanajeshi wake Syria

Sukhoi Su-34 Haki miliki ya picha Russian Defence Ministry
Image caption Ndege za kivita za Urusi zilisaidia sana Rais wa Syria Bashar al-Assad

Urusi imetangaza kwamba itaanza kupunguza wanajeshi wake nchini Syria na itaanza kwa kupunguza meli zake zenye uwezo wa kubeba ndege za kivita.

Tangazo hilo limetolewa na mkuu wa majeshi ya Urusi siku chache baada ya Urusi na Uturuki kufanikisha kupatikana na makubaliano ya kusitisha vita.

Makubaliano hayo yanaheshimiwa, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Urusi imekuwa ikitekeleza mashambulio ya kutoka angani dhidi ya waasi wanaoipinga serikali tangu 2015.

Kushiriki kwa Urusi katika vita hivyo kulimsaidia sana mshirika wake, Rais wa Syria Bashar al-Assad.

"Kwa kufuata uamuzi wa amiri jeshi mkuu wa majeshi ya Urusi Vladimir Putin, wizara ya ulinzi ya Urusi imeanza kupunguza wanajeshi wake Syria," Jenerali Valery Gerasimov amenukuliwa na vyombo vya habari Urusi.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Jeshi la wanamaji likiongozwa na meli ya Admiral Kuznetsov halijatekeleza mchango mkubwa katika vita hivyo

Kamanda wa majeshi ya Urusi nchini Syria Kanali Jenerali Andrei Kartapolov amenukuliwa akisema majukumu yaliyotengewa meli kubwa ya kubeba ndege za kivita ya Admiral Kuznetsov yamekamilishwa.

Hata hivyo, amesema Urusi bado ina uwezo wa kutosha wa kutekeleza mashambulio angani kwa kutumia makombora ya masafa marefu ya kurushwa kutoka ardhini ya S-300 na S-400 ambayo yamewekwa Syria.

Urusi ilitekeleza mashambulio ya kwanza ya angani Syria Septemba 2015, ambapo ilisema ililenga wapiganaji wa Islamic State.

Mwezi Machi, ilitangaza ingeanza kuondoa baadhi ya wanajeshi wake lakini ikaendelea kutekeleza mashambulio ya angani.

Urusi iliondoa baadhi ya ndege wakati huo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii