Barafu kubwa kumeguka Antarctica

ice shelf break up Haki miliki ya picha Adrian Luckman
Image caption Siwa barafu hiyo ina ukubwa sawa na robo ya eneo la Wales

Wanasayansi wameambia BBC kuwa barafu kubwa iliyo na ukubwa mara 50 kushinda kisiwa cha Manhattan, Marekani imefikia kiwango cha kupasuka kutoka eneo kubwa la barafu la Larsen C kaskazini mwa Antarctica.

Siwa barafu hiyo inatarajiwa kuwa miongoni mwa 10 kubwa zaidi zilizopasuka kutoka Antarctica.

Mpasuko mkubwa ulionekana kwenye barafu hiyo ghafla mwezi uliopita na kwa sasa ni sehemu ya kilomita 20 za barafu ambayo inazuia kipande hicho kikubwa cha barafu kumeguka na kuelea baharini.

Larsen C ndiyo sehemu kubwa ya barafu iliyo kaskazini zaidi eneo la Antarctica.

Watafiti walisema iwapo eneo hilo litapoteza kipande hicho cha barafu basi sehemu yote yenyewe itakuwa hatarini ya kupasuka tena siku za usoni.

Eneo la barafu la Larsen C lina kina cha mita 350.

Barafu hiyo huelea maeneo ya pembeni Antarctica Magharibi na kuzuia mito ya barafu ambayo huisaidia kukaa imara.

Watafiti wamekuwa wakifuatilia Larsen C baada ya kumeguka kwa sehemu ya barafu ya Larsen A mwaka 1995 na kisha kupasuka ghafla kwa sehemu ya barafu ya Larsen B mwaka 2002.

Wataalamu wanakadiria kwamba iwapo barafu yote kwenye sehemu hiyo ya bahari ya Larsen C itayeyuka na kuwa maji na kuingia baharini, viwango vya maji baharini vitapanda kwa sentimeta 10.

Haki miliki ya picha NASA
Image caption Ufa kwenye mpasuko wa sehemu hiyo ya barafu una upana wa 100m lakini una kina cha nusu kilometa
Haki miliki ya picha NASA
Image caption Picha zilizopigwa Novemba mwaka jana zikionyesha ufa uliotokea

Mada zinazohusiana