Mlipuko wa bomu wawaua takriban watu 43 Syria

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mji wa Azaz unadhibitiwa na waasi wanaoungwa mkono na Uturuki

Wanaharakati nchini Syria wanasema kuwa bomu lililokuwa limetegwa ndani ya gari limelipuka katika mji ulio kaskazini mwa nchi wa Azaz, na kuwaua takriban watu 43 na kuwajeruhi wengine kadha.

Bomu hilo lililipuka katika soko moja lenye shughuli nyingi kwenye mji unaodhibitiwa na waasi ulio karibu na mpaka na Uturuki.

Azaz umekuwa mji muhimu kwa kupitisha bidhaa kwa waasi.

Islamic State waliudhibiti mji huo wakati mmoja kwa miezi kadha.

Kwa sasa mji huo unadhibitiwa na waasi wanaoungwa mkono na Uturuki. Watu wengi wamechukua hifadhi mjinini humo baada ya kukimbia kutoka mji wa Aleppo mwaka uliopita.