Norway kuzima redio za FM

Oslo Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Vituo vya kitaifa vya redio Norway vitazima mawimbi ya FM kufikia mwisho wa mwaka huu

Norway imekuwa nchi ya kwanza duniani kuzima mawimbi ya redio ya analogu, ambayo yanajumuisha pia masafa ya FM.

Taifa hilo litaanza kuzima masafa ya FM kwa kirefu Frequency Modulation saa 11:11 (saa saba na dakika kumi na moja Afrika Mashariki).

Badala yake, taifa hilo sasa litatumia mawimbi ya dijitali kwa Kiingereza Digital Audio Broadcasting ambayo kwa ufupi yanaitwa DAB.

Mawimbi hayo ya DAB yalianza kustawishwa mwaka 1981 na maonesho ya kwanza ya jinsi teknolojia hiyo inafanya kazi yalifanyika Geneva mwaka 1985.

Mawimbi ya dijitali huwa na ubora zaidi na hufika mbali yakilinganishwa na ya analogu - na gharama yake ni ya chini mno.

Inakadiriwa kwamba gharama yake ni sehemu moja kati ya nane ya gharama ya kawaida.

Lakini kunao walio na wasiwasi kwamba kuzimwa kwa mawimbi hayo kutaathiri wazee na madereva.

Kura ya maoni ambayo matokeo yake yalichapishwa Desemba na gazeti la Dagbladet ilionesha theluthi mbili ya raia wa Norway wanafikiri serikali imeharakisha.

Kufikia mwisho wa mwaka huu, matangazo yote ya redio za taifa nchini humo yatakuwa yakipeperushwa kwa DAB.

Vituo vingine vya kikanda vina miaka mitano kutekeleza mabadiliko hayo.

Na licha ya kwamba asilimia 70 ya wasikilizaji wa redio Norway husikiza kupitia teknolojia ya DAB kwa sasa, wakosoaji wanasema watu wengi watahitajika kutumia pesa nyingi kununua mitambo ya kisasa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Judith Haaland, 98, mkazi wa Stavanger, alikuwa anasikiliza redio kutoka London wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia

Mfano, redio mpya inayotumia teknolojia ya DAB inagharimu karibu NOK4,000 ($468; £382).

Chama cha Vituo vya Redio za Kikanda Norway kinasema ni asilimia 25 pekee ya magari ambayo yana redio za dijitali.

Kunao wengine ambao wanataka kuendeleza kusikiliza FM kutokana na kumbukumbu walizo nazo.

Mawimbi ya FM yalivumbuliwa mwaka 1933 nchini Marekani.

Haki miliki ya picha Thinkstock
Image caption Mataifa mengine pia yanafikiria kuzima mawimbi ya redio ya analogu

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii