Mwili wa aliyekuwa Mfalme Ndahindurwa kuzikwa Rwanda

Msemaji wa familia yake iliyoko Rwanda, mchungaji Ezra Mpyisi
Image caption Msemaji wa familia yake iliyoko Rwanda, mchungaji Ezra Mpyisi

Mwili wa aliyekuwa Mfalme wa mwisho wa Rwanda Kigeli wa Tano Ndahindurwa utazikwa jumapili nchini Rwanda.

Uamuzi huo umetangazwa na familia yake iliyoko nchini Rwanda.

Tangu Mfalme huyo alipofariki akiwa uhamishoni nchini Marekani, familia yake ilikumbwa na mgawanyiko mkubwa kuhusu nchi atakapozikwa na mrithi wake.

Mrithi wake aliyekuwa ameteuliwa na kundi la familia yake lililoko Marekani amekataliwa na kundi linaloishi nchini Rwanda.

Kwa mujibu wa msemaji wa familia yake iliyoko hapa Rwanda,mchungaji Ezra Mpyisi ametangaza kwamba mazishi ya Mfalme wa mwisho wa Rwanda Kigeli wa V Ndahindurwa yatafanyika Jumapili hii eneo la Mwima katika mji wa Nyanza kusini mwa Rwanda.

Amesema kwamba mwili wake utazikwa karibu na kaburi la mkubwa wake Mfalme Mutara Rudahigwa.

Msemaji huyo ambaye ni mshauri wa zamani wa Mfalme amesema shughuli za mazishi zitafuata utaratibu wa kisasa akisisitiza kuwa mambo mengi yalibadilika ikilinganishwa na enzi za kifalme.

Mazishi ya Mfalme Kigeli yanatarajiwa kufanyika mnamo wakati ambapo kundi moja la familia yake lililoko uhamishoni Marekani limetangaza mrithi wa Ufalme ilhali kwa mujibu wa utamaduni wa kifalme mrithi wake hutangazwa siku ya mazishi.

Tangu mfalme huyo afariki akiwa uhamishoni Marekani mwezi wa 10 mwaka uliopita serikali ilijizuiya kuonyesha mkono wake katika kinachoendelea japo baadhi ya taarifa zinasema serikali ilichangia kwa kila jambo.

Hadi kufikia sasa hakuna kinachobainisha ikiwa hafla za mazishi ya Mfalme huyo wa zamani zitakuwa za kitaifa.