Biden atokwa na machozi akipewa medali na Obama

Joe Biden na Barack Obama Haki miliki ya picha AP
Image caption Bw Biden amesema hakutarajia kutunukiwa medali hiyo

Rais wa Marekani Barack Obama amemtunuku makamu wake Joe Biden Medali ya Rais ya Uhuru, ambayo ndiyo nishani ya hadhi ya juu zaidi anayoweza kupewa raia nchini Marekani.

Biden, ambaye alionekana kushangazwa na hatua hiyo, alitokwa na machozi alipokuwa anatunukiwa medali hiyo.

Bw Obama amemsimu makamu huyo wa rais kwa "imani yako katika Wamarekani wenzako, kwa upendo wako kwa taifa na kwa utumishi maisha yako yote."

Tuzo hiyo imetolewa kwa Bw Biden wawili hao wanapojiandaa kuondoka madarakani Donald Trump wa Republican atakapoapishwa kuwa rais mpya tarehe 20 Januari.

Bw Biden amesema anapanga kuendelea kushiriki siasa katika chama cha Democratic.

Hakutarajia

Joe Biden, aliyeonekana kutekwa sana na hisia, alisimama na kuonekana kushangaa Bw Obama alipomlimbikizia sifa na kumtaja kuwa "chaguo bora zaidi, si kwangu tu, bali kwa Wamarekani".

Medali hiyo ilikuwa na hadhi ya ziada, kwa mujibu wa gazeti la New York Times.

Hadhi hiyo ya ziada, katika serikali za Marekani zilizotangulia, ilitunukiwa watu wachache sana, akiwemo Papa John Paul II.

Huwezi kusikiliza tena
Biden atokwa na machozi akipewa medali na Obama

Bw Obama alifanya mzaha kwamba mtandao sasa utakuwa na fursa ya mwisho ya kucheka na kufanyia mzaha kile ambacho kimekuwa kikiitwa "bromance", maana yake upendo na urafiki wa dhati kati ya Obama na Biden.

Kwenye Twitter, watu tayari wameanza kutoa maoni yao.

Haki miliki ya picha Twitter

Wengine wanasema wanaume hao wawili ni mfano bora wa kuigwa katika uhusiano wowote ule.

Haki miliki ya picha Twitter

Bw Biden alisema yeye ni "sehemu ya safari ya binadamu wa kipekee aliyetenda mambo ya kipekee".

Alisema kamwe hakutarajia kwamba angetunukiwa medali hiyo.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Bw Obama alisema kwa mzaha kwamba watu wana fursa ya mwisho kucheka uhusiano wake na Biden

"Sikutarajia kamwe. Nilidhani tulikuwa twaja kwa Michelle kwa ajili yako, Jill na Barack na mimi na watu wengine kadha kufurahia pamoja na kusherehekea safari ambayo tumekuwa nayo pamoja.

"Bw Rais, umegonga ndipo uliposema kwamba nimemtegemea sana Jill lakini nimekutegemea sana, na nimewategemea watu wengine wengi katika chumba hiki.


Medali ya Rais ya Uhuru Marekani

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Diana Ross akitunukiwa Medali ya Uhuru mwaka 2016
  • Ndiyo medali ya hadhi ya juu zaidi anayopewa raia Marekani
  • Ilianzishwa mwaka 1963 na Rais John F Kennedy, ambapo iliizidi Medali ya kawaida ya Uhuru Medal of Freedom
  • Wengi wa waliotunukiwa wamekuwa katika: siasa; biashara; jeshi; muziki; filamu; uanahabari

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii