Palestina: Uhamisho wa ubalozi utaathiri amani

Palestina yafungua ubalozi wake mjini Vatican
Image caption Palestina yafungua ubalozi wake mjini Vatican

Kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas ameonya kwamba amani itaathirika iwapo rais mteule wa Marekani Donald Trump ataidhinisha mpango wa kuuhamisha ubalozi wa Marekani nchini Israel kutoka mjini Tel Aviv hadi Jerusalem.

Alikuwa akizungumza baada ya uzinduzi wa ubalozi wa Palestina katika mji wa Vatican baada ya kukutana na Papa Francis.

Vatican ililitambua taifa la Palestina mwaka mmoja na nusu uliopita.

Swala la Jerusalem ni miongoni mwa maswala yanayovutia hisia kali na tata katika mzozo wote wa mashariki ya kati.

Palestina inalichukulia eneo la mashariki mwa Jeusalem kuwa mji wake mkuu wa taifa lake siku za usoni lakini Israel inalichukuwa eneo hilo lote kuwa mji wake mkuu.

Siku ya Jumapili Ufaransa itaandaa mkutano wa kimataifa mjini Paris ili kujaribu kuanzisha mazungumzo ya amani katika ya pande hizo mbili.