Ndege ya Uturuki yaangukia nyumba Kyrgyzstan na kuua watu 32

Bishkek, Kyrgyzstan (16 Jan 2017) Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Nyumba 15 ziliharibiwa na ndege hiyo

Watu zaidi ya 32 wamefariki baada ya ndege ya kubeba mizigo ya Uturuki, iliyokuwa safarini kutoka Hong Kong, kuangukia nyumba za watu karibu na mji wa Bishkek nchini Kyrgyzstan.

Wengi wa walioangamia ni watu waliokuwa ardhini, maafisa wanasema.

Ndege hiyo aina ya Boeing 747 ilianguka karibu na uwanja wa ndege wa Manas, takriban kilomita 25 kutoka mji mkuu Bishkek, serikali ya Kyrgyzstan imesema.

Nyumba zaidi ya 15 zimeharibiwa na watoto kadha wanaripotiwa kuwa miongoni mwa waliofariki.

Ndege hiyo ilikuwa imepangiwa kutua kwa muda Manas na kisha kuendelea na safari hadi Istanbul, uturuki.

Ndege hiyo inamilikiwa na shirika la ndege za kubeba mizigo la ACT, ambayo hujitambulisha kama MyCargo.

Hata hivyo, serikali ya Kyrgyzstan inasema ndege hiyo ilikuwa inasafiri chini ya shirika la ndege la serikali ya Uturuki,

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Maafisa wanasema chanzo cha ajali hiyo hakijabainika

Maafisa wa shirika hilo hata hivyo wamekanusha taarifa hizo kwenye Twitter.

"Ramirambi zetu kwa jamaa za waliofariki katika ajali hii mbaya iliyohusisha ndege ya shirika la ACT Airlines nchini Kyrgyzstan," Turkish Airlines wameandika.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Kulikuwa na ukungu kutokana na baridi kali

Nyumba kuharibiwa

Ndege hiyo ilianguka mwendo wa saa moja unusu asubuhi saa za huko katika kijiji cha me Dacha-Suu, maarufu sana kwa watalii.

Hali ya hewa ilikuwa mbaya na kulikuwa na ukungu, ingawa chanzo hasa cha ajali hiyo hakijathibitishwa.

Ndege hiyo imekuwa ikifanya kazi kwa miaka 14.

Picha kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha moshi na moto ukifuka kutoka kwenye vifusi vya majumba yaliyoharibiwa.

Kuna taarifa kwamba mhudumu mmoja wa ndege amenusurika.

Kulikuwa na wahudumu wanne kwenye ndege hiyo, maafisa wanasema.

Watu kadha wamepelekwa hospitalini wakiwa na majeraha.

Msemaji wa huduma za dharura nchini humo Muhammed Svarov, ameambia AFP kwamba huenda idadi ya waliofariki ikapanda.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Maafisa wanasema idadi ya waliofariki huenda ikaongezeka

Juhudi za kuwasaka manusura zinaendelea.

Waziri mkuu Sooronbai Jeenbekov amefika eneo hilo sawa na maafisa wa huduma za dharura.

Uwanja mkuu wa ndege wa nchi hiyo wa Manas umefungwa.

Mwaka 2008, ndege ya abiria iliyokuwa safarini kuelekea Iran ilianguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka Manas na kuua watu 68.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii