Mbona magari ni ghali mno nchini Ethiopia?

Magari ni ghali mno nchini Ethiopia
Image caption Magari ni ghali mno nchini Ethiopia

Umiliki wa gari kwa watu wengi nchini Ethiopia, hata kwa watu walio na pesa, kwenye nchi hiyo yenye uchumi unaokua kwa haraka duniani imekuwa ni ndoto tu.

"Nimekuwa nikijiwekea akiba kwa karibu miaka minne sasa, na bado sijafanikiwa kununua gari la bei ya chini kabisa hapa," alisema Girma Desalegn.

Anasema kuwa amekuwa akitafuta gari la kununua kwa wiki nzima mjini Addis Ababa na bado hajapata gari nafuu la kununua.

Lengo lake ni kununua gari ambalo tayari lishatumiwa kutoka mataifa ya Ghuba au Ulaya, lakini bado magari hayo ni ghali kwa sababu serikali imeyaorodhesha magari kama bidhaa za anasa.

Hii inamaanisha kuwa hata kama gari tayari lishatumiwa, litatozwa kodi ya hadi asilimia 300.

Image caption Tatizo kuu nchini Ethiopa ni kodi

"Nina bajeti ya dola 15,000 na nilitarajia kuwa kwa pesa hizo, ningeweza kupata gari zuri la familia, sitaki kununua gari la Toyota Vitz," Desalegn alisema.

Gari la Toyota Vitz hugharimu karibu dola 16,000 nchini Ethiopia huku gari hilo hilo likigharimu bei isiyozidi dola 8000 katika nchi jirani ya Kenya.

Kuvipunguzia kodi viwanda vya ndani

Halmashauri ya kukusanya ushuru nchini Ethiopia inasema kuwa magari ya kibiashara na yale ya kibinafsi yanayoingizwa nchini humo, yanaweza kutozwa aina tano tofauti za kodi.

Hata hivyo licha ya kodi ya juu idadi ya magari yanayoingizwa nchini humo inazidi kuongezeka.

Mwaka 2016, rekodi za serikali zilionyesha kuwa magari 110,000 yaliingizwa nchini Ethiopia, ambalo ni ongezeko la zaidi ya asilimia 50 ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Magari yanayotumiwa kwa usafiri wa umma mara nyingi hupunguziwa kodi

Katika jitihada za kuwawezesha watu kununua magari nafuu yalitotengenezwa nchini Ethiopia, serikali imeyaondolea mzigo wa kodi makampuni ya kigeni ili yaweze kujenga viwanda vya kuunda magari mapya.

Kwa sasa Ethiopia huunda magari 8000 ya biashara na kibinafsi kwa mwaka, kiwango ambacho serikali inakitaja kuwa cha chini.

Waziri mkuu Hailemariam Desalegn, mara kwa mara amesema kuwa Ethiopa ina mipango ya kuwa mzalishaji mkubwa wa magari.

Viwanda kadha vya kigeni vya kuunda magari hasa kutoka China tayari vimejengwa nchini Ethiopia.