Shughuli ya kuitafuta ndege ya MH370 iliyotoweka yasitishwa

Madagascar Haki miliki ya picha Blaine Alan Gibson
Image caption Vipande vimepatikana maeneo ya mbali kama vile Madagascar

Shughuli ya kuitafuta ndege ya shirika la ndege la Malaysia iliyotoweka miaka mitatu iliyopita ikiwa na watu 239 imesitishwa.

Taarifa kutoka kwa Australia, Malaysia na China imesema uamuzi huo umechukuliwa "kwa masikitiko makubwa" baada ya kutofanikiwa kwa juhudi za kutafuta mabaki ya ndege hiyo eneo la ukubwa wa kilomita 120,000 mraba (maili 46,300) katika Bahari ya Hindi.

Jamaa za abiria na wahudumu waliokuwa kwenye ndege hiyo wameshutumu uamuzi huo.

Ndege ya MH370 ilitoweka ikiwa safariki kutoka Kuala Lumpur kuelekea Beijing mwaka 2014.

Kufikia sasa ni vipande saba pekee kati ya vipande 20 vya mabaki ya ndege vilivyopatikana ambavyo vimethibitishwa kuwa vilitoka kwa ndege hiyo aina ya Boeing 777 au kuna uwezekano mkubwa sana kwamba vilitoka kwa ndege hiyo iliyotoweka.

Ripoti moja mwezi Novemba 2016 ilidokeza kwamba huenda ndege hiyo ilishuka kwa kasi kutoka angani na kutumbukia Bahari ya Hindi.

Ndege hiyo ilikuwa na abiria 227 na wahudumu 12, raia wa mataifa 14, ingawa wengi kati yao - watu 153- walikuwa raia wa China.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii