Putin: Taarifa zilizotolewa kuhusu Trump ni 'upuuzi'

Vladmir Putin apuuzilia mbali taarifa zilizofichuliwa kuhusu Donald Trump Haki miliki ya picha AFP
Image caption Vladmir Putin apuuzilia mbali taarifa zilizofichuliwa kuhusu Donald Trump

Rais wa Urusi Vladmir Putin ameyataja madai kwamba taifa lake linashikilia habari muhimu ambazo zinaweza kuathiri uongozi wa rais mteule wa Marekani Donald Trump kama 'upuuzi mtupu'' .

Bw Putin alihoji sababu za kitengo cha ujasusi cha Urusi kumdukua bw Trump kabla ya kuingia katika siasa.

Aliwataja wale wanaotoa madai kama hayo kuwa wabaya zaidi ya ''makahaba''.

Barua zilizochapishwa wiki iliopita zilidai kwamba kundi la uchaguzi la bw Trump lilishirikiana na Urusi ambayo pia inadaiwa kumiliki kanda zake za video kuhusu maisha yake ya kibinafsi.

Madai hayo yanasema kuwa Urusi ina habari mbaya kuhusu biashara za Donald Trump na kwamba bw Trump alirekodiwa na makahaba katika hoteli ya Ritz-Carlton mjini Moscow wakati wa shindano la malkia wa urembo duniani 2013.

Bw Trump amepinga barua hizo zilizodaiwa kuandaliwa na jasusi mmoja wa Uingereza kama ''habari bandia''.