Kuapishwa kwa Trump: Kanye hatatumbuiza sherehe ya Trump

Donald Trump na Kanye West Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Donald Trump alisema alizungumza kuhusu maisha na Kanye West walipokutana Desemba

Kanye West hatatumbuiza wakati wa sherehe ya kuapishwa kwa rais wa 45 wa Marekani, Donald Trump, waandalizi wa sherehe hiyo wamesema.

Kumekuwa na uvumi kwamba tangu nyota huyo wa muziki alipowaambia watu kwamba angempigia Bw Trump kura iwapo angeshiriki uchaguzi, na kisha wakakutana Trump Tower, basi angekuwa mmoja wa wasanii ambao wangetumbuiza Ijumaa.

Lakini Tom Barrack, mwenyekiti wa kamati andalizi ya sherehe ya kuapishwa kwa rais, aliambia CNN kwamba sherehe hiyo si "ukumbi ufaao" kwa West.

Alisema mwanamuziki huyo wa mtindo wa rap ni "jamaa mzuri" lakini "hatujamuomba atumbuize."

Bw Barrack alisema: "Yeye hujichukulia kama rafiki wa rais mteule, lakini huu sio ukumbi wake.

"Ukumbi ambao tunao, upande wa watumbuizaji, umejaa, uko sawa, utakuwa kimsingi wa nyimbo za kitamaduni za Marekani, na Kanye ni jamaa mzuri lakini hatujamuomba atumbuize. Tunaendelea na ajenda yetu."

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii