Wanawake wafanya maandamano ya kumpinga Trump

Waandamana kumpinga Trump
Image caption Waandamana kumpinga Trump

Maandamano ya wanawake dhidi ya Donald Trump, yamefanywa nchini Australia, New Zealand na Japani.

Maandamano makubwa kabisa hadi sasa yamefanywa Sydney, Australia, ambako watu kama elfu tatu wanaopinga ile inayosemekana kuwa tabia ya Bwana Trump, ya kunyanyasa wanawake, waliandamana hadi ubalozi mdogo wa Marekani mjini humo.

Waandamanaji walisema wanataka kumulika haki za wanawake na wachache, ambazo wanasema, zinakabiliwa tishio.

Maandamano zaidi yanayoitwa maandamano ya madada yanapangwa kufanywa sehemu mbali mbali za dunia.

Mkusanyiko mkubwa unatarajiwa mjini Washington, ambako ma-elfu wanatarajiwa kufanya mhadhara.

Baada ya Bwana Trump kuapishwa, maandamano yamefanywa kwengineko na Marekani, pamoja na huko Seattle, ambako mtu mmoja alipigwa risasi na kujeruhiwa.

Mjini Nairobi kundi moja la waandamanaji wakiwemo Wamarekani na raia wa Kenya walikongamana kushiriki katika matembezi ya wanawake ili kupinga unyanyansaji wa kingono na ukosefu wa usawa wa kijinsia mbali na kutaka kushirikishwa katika maswala zaidi ya maendeleo na uongozi.