Mchekeshaji aliyefanyia utani mwana wa Trump, Barron, asimamishwa kazi

Donald Trump Washington. Picha: 20 Januari 2017 Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Barron, 10, (kushoto) ndiye kitinda mimba wa Donald Trump

Mwandishi wa vichekesho wa kipindi cha Saturday Night Live nchini Marekani amesimamishwa kazi baada ya kuandika ujumbe uliomkejeli mwana wa Rais Donald Trump, Barron, kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.

Vyombo vya habari Marekani vimemnukuu mtu anayefahamu mambo ya ndani ya SNL akisema Katie Rich amesimamishwa kazi kwa muda usiojulikana.

NBC, wanaopeperusha kipindi hicho, bado hawajatoa taarifa yoyote rasmi kuhusiana na hilo.

Bi Rich aliandika ujumbe kwenye Twitter Ijumaa akisema: "Barron atakuwa mtu wa kwanza mshambuliaji hapa nchini aliyepokea elimu yake nyumbani."

Ujumbe huo wa mzaha unaonekana kutania suala la matumizi ya silaha Marekani, ambapo kumeripotiwa visa kadha vya raia wa Wamarekani kuwaua watu wengi kwa kuwapiga risasi.

Kinyume na ujumbe unavyoashiria, Barron hahudhurii masomo yake nyumbani bali husomea shule ya kawaida.

Bi Rich alishutumiwa vikali mtandaoni kutokana na ujumbe huo.

Saa chache baadaye aliufuta ujumbe huo na kuufanya ukurasa wake wa Twitter kuwa wa faragha.

Bi Rich alirejea mtandaoni Jumatatu na kuomba msamaha.

Haki miliki ya picha Twitter

Ujumbe mmoja kwenye Facebook wa kujibu ujumbe wa kwanza wa Bi Rich umesambazwa karibu mara milioni tatu kwenye mtandao huo wa kijamii.

Ujumbe huo unasema: "HAKUNA mtoto anayestahili kuzungumziwa kwa njia kama hiyo...Yeye ni mtoto, anafaa kuheshimiwa na hafai kuingiliwa".

Chelsea Clinton, ambaye aliwahi kuishi ikulu kama mtoto, amemtetea Barron.

Haki miliki ya picha Twitter

SNL wameandaa vipindi kadha miezi ya karibuni wakimkejeli Rais Trump.

Bw Trump, aliyeapishwa tarehe 20 Januari, amesema kipindi hicho "hakichekeshi" na waigizaji wake ni "wabaya sana".

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii