UN yainyooshea kidole Israel kuhusu makaazi

Makazi mapya Israel Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Makazi mapya Israel

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea wasiwasi wake juu ya mipango ya Israel ya ujenzi wa makaazi mapya ya nyumba zipatazo elfu mbili na mia tano katika Ukingo wa Magharibi.

Msemaji wa Antonio Guterres amesema hatua ya upande mmoja inaweza kuwa ni kikwazo cha kuelekea amani ya ufumbuzi wa tatizo hilo kwa kuwepo kwa mataifa mawili.

Umoja wa Mataifa unauzingatia ujenzi huo wa makaazi kama siyo halali.

Uamuzi huo ulisisitizwa tena mwezi uliopita katika azimio la Baraza la Usalama ambapo utawala wa Rais aliyemaliza muda wake nchini Marekani Barack Obama uliukataa kwa kupiga kura ya VETO.

Hata hivyo, Waziri mkuu Benjamin Netanyahu na waziri wa ulinzi Avigdor Lieberman wamesema wanakubaliana na hatua hiyo, kutokana na mahitaji ya nyumba yaliyokuwepo.

Kwa upande wa maafisa wa Palestina wanasema mipango hiyo inaondoa matumaini ya kuwepo kwa amani, kutokana na Israel kujenga makaazi yake katika ardhi wanayoitaka kuwa taifa lao la baadaye.

Wasel Abu Yousef mwanachama mwandamizi wa chama cha Wapalestina PLO anataka hatua za kimataifa kuchukuliwa juu ya uamuzi huo wa Israel.

Mwandishi wa BBC mjini Jerusalem amesema serikali ya Israel ni wazi inahisi kutiwa hamasa na Donald Trump, ambaye aliahidi kuwa upande wa Israel zaidi ya mtangulizi wake.