Nchi za Sahel kuunda Jeshi la pamoja kukabili ugaidi

Rais Mahamadou Issoufou Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Rais Mahamadou Issoufou

Viongozi wa nchi tatu za Africa Magharibi wamekubaliana kuunda jeshi la pamoja ili kukabiliana na hali isiyokuwa ya usalama katika eneo la jangwa ambako kuna mipaka ya nchi zao.

Katika taarifa yao ya pamoja walioitoa katika mkutano uliofanyika katika mji mkuu wa Niger, Niamey, viongozi hao kutoka nchi za Burkina Faso, Mali na Niger wamesema eneo hilo kwa haraka linakuwa kimbilio kwa makundi ya kila aina ya ugaidi.

Mwenyeji wa mkutano huo Rais Mahamadou Issoufou amesema jeshi la pamoja la ulinzi litafanya kazi sawa na operesheni za pamoja zinazofanywa na majeshi ya Nigeria, Niger, Chad na Cameroon dhidi ya wapiganaji wa kundi la Boko Haram, katika eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Makundi ya wapiganaji wa kiislamu yenye mafungamano na mtandao wa Al Qaeda, katika siku za hivi karibuni yamefanya mashambulizi katika eneo hilo kwa kupitia sehemu za jangwa.