Mahakama ya Kenya yataka ifichuliwe waliko raia wa Sudan Kusini

Jamaa na marafiki za raia wa Sudan wakiwa mahakamani
Image caption Jamaa na marafiki za raia wa Sudan wakiwa mahakamani

Hali ya wasiwasi ilikuwa imetanda mahakamani hii leo, wakati jamaa na marafiki wa raia wa sudan kusini walipowasilisha mahangaiko yao ya kutoweka kwa raia wawili wa sudan Kusini.

Wakili na mwanaharakati Dong Samuel Luak na mwanachama wa upinzani Aggrey Esbon Idri, walitoweka siku nne zilizopita. Wakili wa familia ya raia hao aliwasilisha madai kwamba huenda raia hao wawili wameshikiliwa chini ya ulinzi mahali ambapo hapajulikani, madai ambayo polisi na idara ya uhamiaji, wamekanusha na kusema kwamba hawana habari yoyote kuhusu kupotea kwa raia hao

Jaji wa mahakama kuu ametoa amri kwamba Idara ya uhamiaji kwamba isiwafukuze nchini raia hao kinyume na sheria na kampuni ya mawasiliano ya simu za mkononi Safaricom itoe ripoti kamili ya mawasiliano ya mwisho ya raia hawa.

Akizungumza na BBC, Rebeca Garang, mke wa marehemu John Garang, amesema kwamba anashangazwa na jinsi mambo yanavyoendelea Juba. Amelazimika kuhamisha mwanawe kutoka Kenya akiwa na hofu kwamba pia analengwa, hii ni baada ya kupatina kwa taarifa kwamba mwanawe ni mmoja wa watu kumi na sita walioorodheshwa na serikali ya Juba kwamba wahamishwe kutoka kenya hadi sudan kusini

shirika la kupigania haki za kibindamu Human Rights Watch, limesema kwamba kwa miaka ya hivi karibuni, Kenya imewafukuza viongozi kadhaa wa upinzani licha ya wao kuorodheswa kama wakimbizi chini ya sheria ya Kenya