Magufuli ahudhuria mkutano wa AU

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Dr John Magufuli

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli, yuko mjini Addis Ababa nchini Ethiopia ambako anahudhuria mkutano wa 28 wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuia ya Umoja wa Afrika (AU).

Hii ndiyo mara ya kwanza ya Rais Magufuli anahudhuria mkutano huo tangu aingie madaraka kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba mwaka 2015.

Akiwa Addis Ababa Rais Magufuli anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Bara la Afrika wanaohudhuria mkutano huo, mkutano ambao pia utahudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Mkutano huo pia utatumiwa kumchagua mwenyekiti mpya wa tume ya Umoja wa Afrika (AU).

Wale wanaowania wadhifa huo wa mwenyekiti ni pamoja na waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Kenya Amina Mohammed, mwanadiplomasia Abdoulaye Bathily kutoka Senegal, waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Chad Moussa Faki Mahamat, mwanasiasa mkongwe kutoka Botswanda Pelonomi Venson-Moitoi na aliyekuwa wakati mmoja mshauri wa rais wa Equatorial Guinea Mba Mokuy.

Haki miliki ya picha AU
Image caption Wawania wa mwenyekiti mpya wa tume ya Umoja wa Afrika (AU).