Trump afanya uteuzi wa jaji mahakama kuu

Trump amesema sifa zake ni za hali ya juu na kwamba atailinda katiba
Image caption Trump amesema sifa zake ni za hali ya juu na kwamba atailinda katiba

Rais wa Marekani Donald Trump amemteua Neil Gorsuch kuziba nafasi iliyoachwa wazi katika mahakama kuu.

Bwana Gorsuch mwenye umri wa miaka arobaini na tisa, ni hakimu katika mahakama ya rufaa mjini Denver.

Wataalamu wanasema Gorsuch hatarajiwi kutoa hukumu kubwa kuhusiana na suala la utoaji mimba na ndoa za watu wa mapenzi ya jinsia moja.

Uteuzi wake utasubiri kuthibitishwa na bunge la senate, ambapo wabunge wa Democratic wametishia kutoka nje iwapo kutakuwa na uteuzi wa mtu anaeonekana kutotaka mabadiliko.

Image caption Gorsuch anahitaji kuthibitishwa kwa wingi wa kura sitini na nne

Kwa upande mwingine, seneta kutoka chama cha Democratic wamezuia kuzipigia kura nafasi tatu za uteuzi wa Trump, ikiwemo waziri wa fedha, afya na mwanasheria mkuu.

Wanahoji, iwapo Jeff Sessions haegemei upande wowote kuweza kuwa mwanasheria mkuu, huku wakisisitiza ni wajibu wao kuhakikisha kwamba wanauchambua kwa kina uteuzi huo.

Kwa upande wake, mkuu wa idara ya usalama nchini Marekani, jenerali John Kelly, ameitetea amri ya kiutendaji ya Rais Trump ya kupiga marufuku ya muda ya kuwazuia wakimbizi pamoja na wasafiri kutoka nchi saba za kiislamu kuingia Marekani.

Kelly amesema amri hiyo imegusa idadi ndogo ya waislamu.