Je, kifo cha Tshisekedi kitaathiri mazungumzo ya amani DR Congo?

Waombolezaji DR Congo Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waombolezaji DR Congo

Wafuasi wa Etienne Tshisekedi kiongozi wa upinzani nchini DR Congo aliyefariki wamekongamana katika mji mkuu wa Kinshasa ili kuonyesha mshangao wao wa kifo cha kiongozi huyo.

Akiwa mpinzani maarufu wa viongozi waliokuja na kuondoka nchin humo alitarajiwa kuongoza baraza la serikali ya mpito kwa makubaliano ya rais Kabila kujiuzulu.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 84 alifariki nchini Ubelgiji ambapo alienda wiki iliopita ili kufanyiwa ukaguzi wa kimatibabu.

Waziri wa habari amesema kuwa atafanyiwa maziko ya kitaifa.

Bw Tshisekedi alirejea mjini Kinshasa mwezi Julai katika makaribisho ya shujaa baada ya kukaa miaka miwili mjini Brussels kwa matibabu ya kiafya.

Kifo chake kinajri wakati muhimu wa DR Congo pamoja na ghasia za maandamano wakati ilipotangazwa kwamba rais Kabila atasalia madarakani hadi mwezi Aprili 2018.

Mwandishi wa BBC nchini DR Congo Anne-Marie Dias Borges anasema kuwa Tshisekedi alikuwa mtu maarufu mjini Kinshasa na kupewa jina la utani la 'Sphinx of Limete'.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Tshisekedi alivutia umati mkubwa katika mikutano yake

Limete ni nyumbani kwake karibu na mji wa Kinshasa.

  • Kipi kitarajiwe katika makubaliano ya amani?

Kifo cha Tshisekedi kinajiri wakati ambapo upinzani na serikali uko katika meza ya kujadiliana kuhusu kuondoka kwa rais Kabila baada ya miaka 16 mamlakani.

Mazungumzo hayo ambayo bado hayajaisha yanahitaji serikali ya mpito pamoja na tarehe ya uchaguzi.

Bw Tshisekedi alitarajiwa kuongoza kamati ya mpito. Amekuwa akipigania demokrasia

Kwa zaidi ya nusu karne sasa taifa lote liliungana nyuma yake dhidi ya uongozi wa kiimla wa Mobutu Sese Seko ama uongozi wa Kabila baba na mwanawe.

Lakini wakati huo bw Tshisekedi alikuwa mnara wa kivyake.

Msimamo wake wakati mwengine huenda ulikuwa kikwazo kwa maendeleo ya kidemokrasia.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliopita Bw Tshisekedi amekuwa akiugua ,mwanawe Felix amekuwa akichukua jukumu kubwa zaidi.

Hatma ya chama cha Union for Democracy and Social Progress UDPS inayumbayumba.

Viongozi wengine wachanga wa upinzani sasa wanaweza kupata fursa ya kuingia katika mazungumzo hayo ya mpito ambayo yanatarajiwa kuendelea chini ya uongozi wa viongozi wa makanisa nchini humo.

  • Je, watu wamepokea vipi kifo chake?

Mashahidi wanasema kuwa huku habari za kifo chake zikiendelea kusambaa mjini Kinshasa siku ya Jumatano jioni, ghasia zilizuka kati ya kundi moja la wafuasi wake na maafisa wa polisi ambao walitumia vitoa machozi.

Waombolezaji waliokongamana katika nyumba ya mwanawe mjini Kinshasa wanasema wana wasiwasi kuhusu hali ya baadaye.

''Mtu huyo alijitolea maisha yake pamoja na ujana wake wote.Mtu huyu alitufanya tufungue macho, alikuwa shujaa wetu''.

''Alikuwa taa ya Afrika. Alikuwa maarufu.Tumepoteza mtu muhimu sana'', mwanamke mmoja aliambia BBC.

Mwengine anasema wafuasi wake walikuwa wanamjua kuwa mtu ambaye ilikuwa vigumu kumhonga.

''Alikuwa mpinzani wa kihistoria.Mandela alikuwa wa kwanza na Tshisekedi alimfuata''.

Waziri wa maswala ya kigeni nchini Ubelgiji Didier Reynders alimtaja Tshisekedi kama mwanasiasa maarufu.

Ubelgiji inajiunga na raia wa DR Congo katika wakati huu wa huzuni ili kuona kwamba kazi yake inazaa matunda, kilisema chombo cha habari cha AFP.

  • Ufanisi wake ni nini katika miaka 57 ya siasa?

Akiwa mzaliwa katika jimbo la kati la Kasai mnamo mwezi Disemba mwaka 1932, bw Tshisekedi akiwa na umri wa miaka 79 alikuwa kiongozi wa upinzani mwenye umri mkubwa.

Alisomea sheria chini ya ukoloni nchini Ubelgiji.

Harakati zake za kisiasa zilianza wakati wa uhuru wa taifa hilo mwaka 1960 ambapo alikabidhiwa nyadhfa za juu katika serikali ya kati mbali na utawala wa Kasaian uliokuwa mfupi.

Mnamo terehe 14 mwezi Novemba 2011, akiwa waziri wakati wa serikali ya dikteta Mobutu Sese Seko bw Tshisekedi alijimwaga katika siasa za upinzani 1980 wakati Mobutu alipoamua kufutilia mbali uchaguzi wote.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mobutu Sese Seko

Akiwa kiongozi wa chama cha muungano wa Demokrasia pamoja na chama cha Social Progrees, amekuwa mpinzani wa serikali zote tangu wakati huo.

Wakati Mobutu alipolazimishwa kutengeza serikali ya muungano na upinzani, bw Tshisekedi alikuwa waziri mkuu mara mbili katika kipindi cha miaka miwili.

Alijiuzulu nyakati zote hizo alipokosana na Mobutu.

Chama cha Bw Tshisekedi hakikushiriki katika vita wakati wa vita vilivyozuka baada ya utawala wa Mobutu kuanguka 1997, na hivyobasi kupata umaarufu mkubwa kutoka kwa raia walioathirika na mapigano hayo.

Baada ya kususia uchaguzi mwaka 2006, ambao anadai ulifanyiwa udanganyifu ,bw Tshisekedi aliamua kujitokeza na kuhakikisha kuwa anashinda.

Kwa wengine aliamua mapema kujitangaza kuwa rais kabla ya kupigwa kwa kura hiyo.