Mahakama yakataa rufaa ya Trump

Amri ya Trump imesababisha maandamano makubwa Haki miliki ya picha AFP
Image caption Amri ya Trump imesababisha maandamano makubwa

Mahakama ya rufaa nchini Mareni imekataa ombi kutoka kwa idara ya haki nchini humo la kutaka kurejeshwa amri ya Trump ya kupiga marufuku wasafiri kutoka nchi saba zenye waislamu wengi kuingia Marekani.

Serikali ilikuwa imeitaka mahakama kurejesha amri hiyo baada ya uamuzi wa jaji kwenye mahakama ya Seatttle wa kupiga marufuku amri hiyo.

Bwana Trump alikashifu uamuzi huo wa jaji akisema kuwa unaiweka Marekani kwenye hatari ya kushambuliwa na magaidi.

Mashirika makubwa ya usafiri wa ndege, yangali bado yanawakubalia raia kutoka mataifa hayo husika, kuabiri ndege na kuingia Marekani.

Kumekuwepo na maandamano dhidi ya marufuku hiyo ya Trump huko Washington, jimbo la Miami na miji mingine kadhaa ya Marekani, pamoja na miji mingine mikuu ya bara Ulaya.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Trump

Wakati huo huo, Rais Trump ametetea uhusiano wake na Rais Vladimir Putin, katika mahojiano ya Runinga, huku akikataa kupinga madai ya mtangazaji kuwa Rais huyo wa Urusi ni muuaji.

Katika mahojiano ambayo yatapeperushwa na runinga ya Fox News baadaye leo Jumapili, Bwana Trump ameashiria kuwa Marekani isijifanye kutokuwa na hatia, kwani pia ina wauaji wengi.

Amesema kuwa anamheshimu Bwana Putin, na itakuwa jambo bora zaidi ikiwa Urusi itasaidia Marekani kupambana na wanamgambo wa kundi la Islamic State.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Wasafiri kutoka mashariki ya kati wawasili Los Angels