Buhari aongeza muda wa kupata matibabu zaidi Uingereza

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais wa Nigeria

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amelitaka bunge la nchi hiyo kumuongezea likizo yake, ya kupata matibabu.

Ametoa taarifa hiyo akiwa nchini Uingereza kwa ajili ya vipimo vya afya yake.

Rais Buhari aliondoka nchini Nigeria wiki mbili zilizopita na alitarajiwa kurudi mjini Abuja jana.

Taarifa iliyotolewa na ofisi yake imesema, ameshauriwa na madaktari kumaliza matibabu na kusubiri matokeo ya vipimo alivyopima.

Wadadisi wanasema kuwa kuongezwa kwa muda huo wa Buhari kusalia Uingereza huenda kukahujumu imani kwa uongozi ambao tayari uko chini ya shinikizo la uchumi mbaya na mzozo kutoka kwa kundi la Boko Haram kaskazini mashariki mwa nchi.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kundi la Boko Haram ni moja ya matatizo yanayoikumba Nigeria

Nigeria kwa sasa inakabiliwa na hali mbaya zaidi ya uchumi tangua miaka kadha, kufuatia kushuka kwa kiwango kikubwa bei ya mafuta ambayo ni tegemeo la uchumi.

Biashara na wawekezaji wanalalamika jinsi serikali imelishughulikia suala la sarafu za kigeni, hatua ambayo imesababisha hali kuwa mbaya zaidi.

Makamu wa rais Yemi Osinbanjo anachukua majukumu ya rais wakati Buhari akiwa ng'ambo.