Taarifa ya habari kwa ufupi

Taarifa ya habari na Dinah Gahamanyi
Image caption Taarifa ya habari na Dinah Gahamanyi

* Rais Donald Trump amesema kuwa amewawaagiza maafisa wa mpaka kuwafanyia uchunguzi watu wanaoingia nchini Marekani kwa umakini zaidi , wakati marufuku aliyoweka dhidi ya wasafiri kutoka nchi saba hususan za kiislam ikiwa imeahirishwa . Amesema kuwa mahakama ambazo zilizuwia marufuku hiyo zinafanya ulinzi wa mipaka mwa Marekani kuwa mgumu na amewashutumu majaji waliowezesha uamuzi kwa kuiweka nchi katika hatari .

* Takriban watu nusu milioni wanakadiriwa kushiriki Maandamano makubwa yanayoendelea nchini Romania kwa usiku wa sita mfululizo , licha ya kwamba serikali imeondoa sheria ambayo ingehalalisha baadhi ya makosa ya ufisadi.

* Watafiti nchini Uingereza wamebaini kuwa makundi yenye itikadi kali kama Islamic State yanawaingiza kwenye makundi hayo watoto wanaokimbia mizozo wakiwa peke yao. Uchunguzi huo uliofanywa na wakfu unaochunguza fikra za itikadi kali unasema kuwa makundi hayo yanajaribu kuvutia ufuasi wa watoto katika kambi za wakimbizi kwa kuwalipa watu wanaowatorosha na kuwasafirisha hadi ulaya

*Maafisa wa kanisa katoliki nchini Australia wanatarajiwa kufikishwa mbele ya tume maalum inayochunguza unyanyasaji wa watoto ili kutoa sababu za majibu yao kuhusiana na unyanyasaji wa kijinsia waliofanyiwa watoto na makasisi . Maaskofu sita wameitwa mjini Sydney kufafanua ni kwa nini unyanyasaji wa watoto wengi umekuwa ukiendelea kwa miongo mingi

* Sherehe kubwa zimekuwa zikiendelea nchini Cameroon baada ya timu ya taifa ya soka ya taifa hilo kushinda kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Misri . Maelfu ya mashabiki walipeperusha bendera ya nchi yao na kucheza ngoma na densi kwenye mitaa ya mji mkuu , Douala, wakishangilia na kupuliza pembe

*Mojawapo ya tukio la michezo ya mwaka inayopendwa zaidi nchini Marekani , the Super Bowl, linafanyika katika mji wa Houston. Timu ya Soka ya The New England Patriots ya Marekani inacheza na the Atlanta Falcons - ambao wameongoza katika kipindi cha kwanza wakiwa na azma kuchukua taji la Super Bowl kwa mara ya kwanza . Nyota wa muziki wa pop Lady Gaga amekuwa jukwaani kama mtumbuizaji mkuu katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo.