Maaskofu wahojiwa kuhusu unyanyasaji wa kingono Australia

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani papa Francis
Image caption Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani papa Francis

Maafisa wa kanisa lenye ushawishi zaidi la Katoliki nchini Australia wataanza kufika mbele ya tume maalum inayochunguza unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto uliofanywa katika kanisa hilo .

Maaskofu sita wameitwa na tume hiyo kufafanua majibu yao kuhusu unyanyasaji wa jinsia uliofanywa na makasisi dhidi ya watoto .

Tume hiyo ya kitaifa iliundwa mwaka 2013 kuchunguza madai ya unyanyasaji huo katika taasisi zote nchini Australia , zikiwemo shule, vilabu vya michezo na mashirika ya dini .

Viongozi wa ngazi ya juu wa kanisa nchini Australia watatakiwa kutoa maelezo juu ya ni kwa vipi unyanyasaji huo wa kijinsia wa watoto uliendelea kwa kipindi cha miongo mingi .

Pia wataiambia tume hiyo mjini Sydney ni hatua gani ambazo zimechukuliwa na kanisa katoliki kuhakikisha unyanyasaji wa kijinsia wa watoto haurudiwi tena.

Mmoja wa maaskofu wakuu tayari amekwisha kuahidi kumaliza uovu huu .

Tume hiyo inatarajiwa kuchapisha ripoti yake ya mwisho mnamo mwezi Disemba , takriban miaka mitano baada ya kuanza kuchunguza maelfu ya madai ya unyanyasaji wa kingono na kimwili kwa ujumla unaodaiwa kutekelezwa katika taasisi mbali mbali za kidini kote nchini Australia.