Sudan Kusini yaonywa, mapigano kusababisha maafa zaidi

Vita kusababisha maafa zaidi Sudan
Image caption Vita kusababisha maafa zaidi Sudan

Umoja wa Mataifa umeonya juu ya mapigano yanayoendelea Sudan kusini kuwa yanaweza kusababisha maafa zaidi.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulika na kuzuia mauaji ya watu wengi, Adama Dieng amesema zaidi ya watu elfu 52 wamekimbilia nchini Uganda katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita pekee na wamekuwa wakizungumzia mauaji ya raia, uharibifu wa nyumba na unyanyasaji wa kijinsia unaofanywa wakati wa mapigano hayo.

Amesema binafsi ameshtushwa na hali ilivyo katika mji wa Kajo -keji ulioko kusini mwa mji mkuu wa nchi hiyo Juba, ambako kikosi cha Walinzi wa Usalama wa Umoja wa Mataifa walifika huko siku ya Jumapili.

Baada ya kupata uhuru wake mwaka 2011 Sudan ya kusini iliingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013 na kusababisha watu takriban milioni tatu kuyakimbia makazi.

Zaidi ya watu milioni sita, nusu ya idadi ya watu wa nchi hiyo inasemekana wanahitaji msaada wa haraka.