Ndege ya Pakistan yalazimishwa kutua Uingereza

Polisi wakiingia ndani ya ndege, mara tu ilipowasili katika uwanja wa Stansted Haki miliki ya picha Rex Features
Image caption Polisi wakiingia ndani ya ndege, mara tu ilipowasili katika uwanja wa Stansted

Ndege za kivita za jeshi la angani la Uingereza, zimeielekeza ndege moja ya abiria kutoka Pakistan, ambayo ilikuwa itue Heathrow, hadi uwanja wa ndege wa Stansted.

Taarifa kutoka Stansted, zinasema kuwa ndege hiyo iliyokuwa ikitokea mji wa Lahore hadi Heathrow, ilikuwa imetua Essex saa tano na dakika hamsini, saa za Afrika Mashariki, na ndipo hatua hiyo ikaamuliwa.

Msemaji wa Polisi huko Essex amesema: "Ndege hiyo ilibadilishwa mkondo hadi uwanja wa ndege wa Stansted mwendo wa saa 12 jioni saa za Afrika mashariki ikiwa bado juu ya anga ya Uingereza ikiwa inaelekea uwanja wa ndege wa Heathrow baada ya kupokea taarifa ya kuwepo kwa abiria msumbufu ndani ya ndege." Akasema msemaji huyo, huku akiongeza kuwa "haikubainika mara moja iwapo lilikuwa tishio la utekaji ndege nyara au swala la ugaidi".

Haki miliki ya picha FLIGHTRADAR24.COM
Image caption Flightradar24.com ilifuatilia njia ya ndege hiyo ikiwa juu ya anga ya Uingereza

Kutokana na swala ambalo halihusiani na hili, abiria mmoja alikuwa akamatwe na maafisa wa polisi mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Heathrow Jijini London na badala yake akazuiliwa uwanjani Stansted.

Duru kutoka kwa polisi jijini London, zinasema kuwa, mtu huyo mwenye umri wa miaka 52 amekamatwa kwa kushukiwa kuwa, alikuwa akipanga kutekeleza makosa ya ufisadi nchini Uingereza, na amehamishiwa hadi katika kituo cha Polisi cha London.

Mamlaka kuu ya ndege nchini Pakistan iliandika katika mtandao wake wa tweeter: "#PIA ndege inayoelekea Heathrow kutoka Lahore, imebadilishwa mkondo hadi #Stansted kwa sababu ya hali ilivyo ndani ya ndege."

Haki miliki ya picha PA
Image caption Arfah Khawaja, kutoka Pakistan. ambaye alikuwa kwenye ndege hii, amesema kuwa hakukuwa na ishara yoyote ya matatizo

Arfah Khawaja, pia alisema kuwa baada ya ndege kutua hali haikuwa shwari kabisa, "Ilikuwa hali ya kutamausha na yenye kutia hofu"

Anasema kuwa abiria walikuwa ndani ya ndege uwanjani Stansted kwa muda wa saa sita, kufuatia safari hiyo ya masaa manane tu kutoka Lahore hadi Heathrow.

Mwanadada huyo amesema kuwa, askari wanane waliokuwa wamejihami vilivyo na silaha, walimtoa kwa nguvu mwanamume mmoja ndani ya ndege.

Ndege hiyo aina ya Airbus A330, inalindwa baada ya hatua hiyo, huku shirika la ndege la Pakistan likisema kuwa abiria wamepewa "usafiri wa ardhini" hadi London.

Muda wote wa kizaa zaa hicho, uwanja wa ndege wa Stansted ulikuwa ukifanya kazi.