Uchaguzi wa Somalia waingia raundi ya pili

Wabunge wakipiga kura katika eneo la kuwekea ndege ndani ya uwanja wa ndege wa Mogadishu Haki miliki ya picha AMISOM
Image caption Wabunge wakipiga kura katika eneo la kuwekea ndege ndani ya uwanja wa ndege wa Mogadishu

Mwandishi wa BBC mjini Mogadishu alichapisha ujumbe wa Twitter kwamba aliyekuwa waziri mkuu Mohamed Abdullahi Farmajo ameshinda raundi ya pili ya uchaguzi huo.

Anasema kuwa baadhi ya watu wameanza kushangilia lakini ripoti za hivi punde zinasema kuwa hajapata thuluthi mbili ya kura hizo.

Hatua hiyo inamaanisha kwamba uchaguzi huo utaendelea kwa raundi nyengine ya tatu

Kabla ya raundi hiyo waziri mkuu Omar Abdirashid Ali Sharmarke alijiondoa katika uchaguzi wa kuwania urais na kuwawacha wagombea watatu katika raundi ya pili .

Wagombea hao ni Hassan Sheikh Mohamud aliyejipatia kura 88,Mohammed Abdullahi Mohamed farmajo akipata kura 72.

Aliyekuwa rais wa zamani Sharif Sheikh Ahmed alipata kura 49.

Vilevile milio ya risasi imedaiwa kusikika katika maeneo tofauti karibu na uwanja huo wa ndege wa mji mkuu wa Mogadishu.

Awali wabunge nchini humo walipiga kura kumchagua rais wa taifa hilo katika uwanja wa ndege ambapo usalama umeimarishwa mjini Mogadishu kwa kuwa maeneo mengine ya mji huo sio salama.

Milolongo ya magari ilipigwa marufuku na shule kufungwa huku ndege zikipigwa marufuku kuingia ama hata kutoka mjini Mogadishu ili kuzuia shambulio lolote.

Licha ya hayo yote wapiganaji wa al-Shabab walirusha makombora karibu na eneo la uchaguzi huo usiku wa Jumanne.

Taifa la Somalia linalokabiliwa na vita vya kikabila pamoja na vile vya ukoo halijafanikiwa kufanya uchaguzi wa kidemokrasia unaoshirikisha raia kushiriki katika uchaguzi tangu 1969.

Uchaguzi huo ulifuatiliwa na mapinduzi ,uongozi wa kiimla na vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoshirikisha koo na wapiganaji wa al-Shabab.

Uchaguzi huo unaonekana kama mojawapo ya harakati za kujenga tena demokrasia mbali na kuweka uthabiti.

Haki miliki ya picha AMISOM
Image caption Usalama umeimarishwa katika maeneo mbali mbali ya mji wa Mogadishu

Zaidi ya wanajeshi 20,000 wa Umoja wa Afrika wako nchini Somalia ili kuzuia kundi la wapiganaji wa al-Shabab kuipindua serikali dhaifu ya taifa hilo.

Takriban wagombea 20 wanawania wadhfa huo wa urais , huku watatu kati yao wakitarajiwa kusonga mbele kwa raundi ya pili ya upigaji kura ambapo wagombea watakaokuwa wa kwanza na wa pili wataingia katika raundi ya tatu ya kura ya mwisho.

Eneo na uwanja huo linalopigiwa kura ni eneo la kuwekea ndege na limejaa wabunge kulingana na mwandishi wa BBC Ferdinand Omondi aliyeko huko.

Rais Hassan Sheikh Mohammud anatetea wadhfa wake na wachanganuzi wanasema kuwa huenda akawa miongoni mwa wagombea watakaofuzu katika raundi ya pili na ya tatu.

Uwanja huo wa ndege unaonekana kuwa eneo pekee lenye usalama mkubwa na uchaguzi huo unafanyika hapo baada ya kuondolewa katika taasisi ya mafunzo ya polisi kutokana na wasiwasi wa kiusalama.

Image caption Ramani ya taifa la Somalia

Siku ya Jumanne jioni, watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa al-Shabab walitekeleza msusuru wa mashambulio huku makombora yakirushwa karibu na eneo la uchaguzi huo.

Wakaazi katika kijiji cha Arbacow nje ya Mogadishu wanasema wapiganaji wa Jihad walishambulia kambi ya Umoja wa Afrika katika eneo hilo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii