Maseneta wamuidhinisha mwanasheria mkuu wa Trump Jeff Sessions

Jeff Sessions Haki miliki ya picha AFP
Image caption Jeff Sessions ni miongoni mwa waliomuunga mkono Donald Trump mapema

Bunge la Seneti nchini Marekani limeidhinisha mtu aliyeteuliwa na Rais Donald Trump kuwa mwanasheria mkuu wa nchi hiyo, Seneta wa Alabama Jeff Sessions.

Ameidhinishwa kwa kura 52 dhidi ya 47.

Ameidhinishwa baada ya vikao vilivyojaa majibizano makali ambapo maseneta wa chama cha Democratic walikosoa sana historia ya Bw Sessions kuhusiana na kuheshimu haki za kiraia.

Seneta wa Democrat Elizabeth Warren alinyamazishwa kwa kufufua madai ya ubaguzi wa rangi aliyodaiwa kuyatenda Bw Sessions.

Miongoni wa watu walioteuliwa na Bw Trump, uteuzi wa seneta huyo wa Alabama uliokuwa miongoni mwa uliozua utata zaidi.

Maseneta wengi sana walipiga kura kwa kuegemea vyama vyao.

Ni seneta mmoja pekee wa Democratic aliyempigia kura Sessions, seneta wa West Virginia Joe Manchin.

Wenzake Sessions katika Seneti wa chama cha Republican walimsifu sana na wingi wao ulihakikisha kwamba anaidhinishwa.

Sasa, atakuwa kiongozi wa Wizara ya Haki ambayo ina wafanyakazi 113,000, wakiwemo wanasheria 93.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii