Kenya: Mahakama yapinga hatua ya kufunga kambi ya wakimbizi Dadaab

Wakimbizi katika kambi ya Dadaab
Image caption Kambi ya Dadaab ndiyo kubwa zaidi duniani

Mahakama Kuu nchini Kenya imebatilisha uamuzi wa serikali ya Kenya wa kufunga kambi kubwa ya wakimbizi ya Daadab inayopatikana kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Mahakama imesema waziri wa usalama wa ndani Meja Jenerali mstaafu Joseph Nkaissery alikiuka katiba wakati wa kutoa agizo la kufungwa kwa kambi hiyo.

Jaji JM Mativo amesema agizo la serikali lilibagua na lilikuwa sawa na kuadhibu watu kwa pamoja.

Jaji huyo alikuwa anatoa uamuzi katika kesi iliyowasilishwa na mashirika mawili ya kutetea haki za kibinadamu: Shirika la Taifa la Haki za Kibinadamu na Kituo Cha Sheria, yakisaidiwa na shirika la kimataifa la Amnesty International.

Serikali awali ilitangaza kwamba ingefunga kambi hiyo, ambayo ndiyo kubwa zaidi duniani, tarehe 30 Novemba mwaka 2016. Ilisema hatua hiyo ilifaa ili kulinda Kenya dhidi ya mashambulio ya kigaidi.

Hata hivyo, iliongeza muda wa miezi sita "kwa sababu za kibinadamu".

Kambi hiyo inatoa hifadhi kwa wakimbizi 260,000, wengi kutoka Somalia.

Shirika la Amnesty International linasema wengi wa wakimbizi hawana pa kwenda.

Ripoti ya shirika hilo iliituhumu serikali kwa kuwashurutisha wakimbizi hao kurejea Somalia kinyume na mapenzi yao.

Mkurugenzi wa shirika hilo Afrika Mashariki na eneo la Maziwa Makuu Muthoni Wanyeki ametaja uamuzi wa leo wa mahakama kuwa wa kihistoria.

"Uamuzi huu unasisitiza wajibu wa Kenya kuheshimu katiba na sheria na mikataba ya kimataifa kwa kulinda watu wanaotafuta hifadhi na kutoroka mateso," amesema.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii