Mahakama yapinga kufungwa kwa kambi ya Daadab

Kambi ya wakimbizi ya Dadaab
Image caption Kambi ya wakimbizi ya Dadaab

Mahakama kuu nchini Kenya imezuia mpango wa serikali wa kutaka kuifunga kambi kubwa ya wakimbizi duniani ya Dadaab karibu na mpaka na Somalia mbali na kuwarudisha nyumbani wakimbizi wa Somalia.

Jaji wa mahakama hiyo aliamuru kwamba uamuzi huo wa kuwaondoa kwa lazima wakimbizi hao ni sawa na kuwatesa na hivyobasi ni kinyume na sheria.

Serikali ilitoa agizo hilo la kuifunga kambi hiyo mwaka uliopita, ikisema ni muhimu kulilinda taifa kutokana na vitisho vya kiusalama.

Imelishtumu kundi la wapiganaji wa kiislamu al-Shabab kwa kutekeleza operesheni zake kutoka kambini humo.

Hatahivyo, tarehe ya mwisho ya kufungwa kwake ilipelekwa mbele hadi mwezi Mei, ikisubiri majadiliano.

Makundi mawili ya wanaharakati baadaye yaliwasilisha kesi mahakamani yakipinga hatua hiyo ambayo yamedai ni ya kibaguzi na kinyume na sheria ya kimataifa.

Dadaab inawahifadhi zaidi ya watu 300,000.