Hasara ya mtandao wa Twitter yaongezeka maradufu

Mtandao wa Twitter waripoti hasara kubwa Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mtandao wa Twitter waripoti hasara kubwa

Hisa katika kampuni ya Twitter zinatarajiwa kushuka baada ya kutangaza kuwa hasara yake ya robo ya nne imeongezeka maradufu.

Kampuni hiyo imeripoti hasara ya dola milioni 167 katika miezi mitatu ya mwisho ya mwaka 2016 ,dhidi ya dola milioni 90 katika kipindi kama hicho mwaka 2015.

Twitter ilikuwa na wateja milioni 319 ikiwa ni asilimia 4 lakini mapato ya matangazo yakashuka kidogo hadi dola milioni 638.

Donald Trump ambaye ni mteja wa mtandao huo hakuimarisha mapato yake licha ya kuutumia wakati wa kampeni yake.

Mapato ya robo ya nne ya mwaka yalikuwa dola milioni 717,ikiwa ni asilimia 1 juu ya mapato ya mwaka jana ya dola milioni 710.

Mapato na idadi ya wateja wa mtandao huo yalipungua.

Baadhi ya wachanganuzi walitaraji kwamba utumizi wa Twitter wa rais mpya Donald Trump ungeipiga jeki huduma hiyo.

Lakini katika makutano na vyombo vya habari afisa wa opreresheni katika kampuni hiyo Anthony Noto alifutilia mbali wazo hilo kwamba athari ya Trump ilikuwa muhimu sana katika kuongezeka kwa idadi ya watumiaji wa mtandao huo.

Alisema kuwa ijapokuwa Trump alionyesha uwezo wa Twitter na kupanua hamasa ya mtandao huo ingekuwa vigumu kwa mtu mmoja kuleta tofauti kama hiyo.