Eman Ahmed: Mwanamke mwenye kilo 500 kutoka Misri apelekwa India

Eman Ahmed Haki miliki ya picha AP
Image caption Eman Ahmed hajasafiri kwa muda wa miaka 25

Mwanamke raia wa Misri, ambaye inasadikika kwamba ndiye mwenye uzani wa juu zaidi duniani, amewasili mjini Mumbai nchini India kufanyiwa upasuaji.

Eman Ahmed Abd El Aty mwenye umri wa miaka 36 ana uzani wa kilo 500 na anahitaji kufanyiwa upasuaji kumsaidia kupunguza uzani wake.

Safari hiyo ya Jumamosi ilikuwa mara yake ya kwanza kwake kuondoka nyumbani katika kipindi cha miaka 25.

"Eman aliyesafiri kwa ndege ya EgyptAir aliwasili katika uwanja wa ndege wa Mumbai majira ya saa kumi alfajiri na akafika hospitalini Saifee mwendo was aa kumi na mbili alfajiri. Kitanda maalum alicholalia kiliinulia, yeye akiwa bado kitandani, kwa kutumia kreni," madaktari walisema.

Alisafirishwa hadi hospitalini kutoka uwanja wa ndege kwa kutumia lori maalum ambalo lilifuatwa na gari la kuwabebea wagonjwa pamoja na gari la polisi.

Katika hospitali ya Saifee, kuna chumba kilichojengwa mahsusi kwa ajili yake.

Atakuwa chini ya uangalizi wa madaktari kwa muda wa mwezi mmoja kabla ya kufanyiwa upasuaji, madaktari wamesema.

Kwa sasa atatunzwa na mtaalamu wa upasuaji Muffazal Lakdawala na kundi lake la matabibu, ambao wamekuwa wakimtunza kwa karibu miezi mitatu na walifanikisha kusafirishwa kwake kutoka Misri.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Eman Ahmed akiinuliwa pamoja na kitanda chake

Kutokana na hali kwamba hajatoka kitandani kwa miaka 25 iliyopita, kulikuwa na hatari kwake kuugua maardhi ya kupumua aksafirishwa na madaktari walichukua tahadhari kubwa na kumpa dawa za kuyeyusha damu mwilini.

Kitanda alichosafirishwa nacho ni kitanda maalum kilichoundwa na mafundi wa Misri kwa kufuata matakwa ya shirika la ndege la EgyptAir.

Kilikuwa na mitambo na vifaa vya huduma ya dharura.

Familia ya Eman Ahmed inasema kuwa alikuwa na uzani wa kilo 5 alipozaliwa kabla ya kupatikana na ugonjwa wa matende, ugonjwa ambao unasababisha kufura kwa mwili kutokana na maambukizi ya vimelea.

Wakati alipofikisha umri wa miaka 11, uzani wake uliongezeka maradufu na akaugua kiharusi ugonjwa uliomuacha kitandani kwa kipindi kirefu cha maisha yake.

Daktari wa upasuaji wa kupunguza matumbo kwa lengo la kutaka kupunguza uzani Muffazal Lakdawala hata hivyo aliambia BBC mwezi Desemba kwamba anaamini Eman Ahmed haugui ugonjwa wa matende lakini anaugua ugonjwa wa kunenepa kupita kiasi ambao husababisha miguu kuvimba.

Ubalozi wa India mjini Cairo ulikuwa umemkatalia kupewa visa bi Abd El Aty kwa kuwa hakuweza kusafiri pekee.

Haki miliki ya picha Image copyrightCOURTESY: DR MUFFAZAL LAKDAWALA
Image caption Eman Ahmed Abd El Aty mwenye ana umri wa miaka 36

Alipewa visa baada ya Dkt. Lakdawala kutuma ujumbe katika Twitter kwa waziri wa maswala ya kigeni nchini India Sushma Swaraj ambaye alijibu kwa ombi la kutaka kutoa usaidizi.

Upasuaji wa kupunguza matumbo ili kupunguza uzani wa mtu aliye na uzani mkubwa hutumika kama hatua ya mwisho ya kuwatibu watu walio na uzani mkubwa na walio na mafuta mengi.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii