Waandishi washtakiwa Ivory Coast

Ivory coast
Image caption Nembo ya mahakama ya kimataifa

Waandishi sita nchini Ivory Coast wameshtakiwa kwa kueneza habari potofu hivyo kuhatarisha usalama wa taifa.

Washtakiwa hao sita, ni waandishi na wahariri ambao jarida lao limechapisha makala kuhusu uasi uliofanywa wiki iliyopita na vikosi maalum vya nchi hiyo. Waandishi hao wameripoti kwamba vikosi maalum viliomba fedha nyingi ili kusitisha uasi wao.

Lakini serikali imedai wanajeshi hao walirudi kazini bila kuwepo kwa masharti yoyote, na kuongeza kusema kwamba pia wanajeshi hao waliomba radhi kwa mgomo wao wa siku mbili uliofanyika katika kambi ya Adiake karibu na mpaka wa Ghana.

Waandishi hao, wanaofanya kazi katika gazeti la kujitegemea, wameripoti kwamba wizara ya ulinzi umewalipa waasi hao kurudi kazini.

Wameachiwa baada ya kuwepo kizuizini kwa siku mbili. Lakini mashtaka wanayokabiliwa nayo ya kuhatarisha usalama wa taifa, hukumu yake inaweza kuwa kifungo cha mpaka miaka mitano. Uasi wa kwanza ulianza mwezi jana katika mji mkuu wa Bouake na hatimae kuenea nchi nzima.