Donald Trump ana mpango gani kuhusu amani ya pande mbili?

Netanyahu anakutana na Donald Trump nchini Marekani Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Afisa wa ikulu ya Rais Marekani amesema kuwepo kwa nchi mbili huru siyo suluhu pekee la kupatikana amani kati ya Israel na Palestina.

Kauli hii imetolewa wakati viongozi wa Israel na Marekani wakikutana kwa mara ya kwanza tangu kuchaguliwa kwa Donald Trump kama Rais wa Marekani.

Bwana Trump ameelezea matumaini ya majaliwa ya amani kati ya Israel na Palestina ambayo yameonekana kungonga mwamba.

Aidha amesisitiza kuunga mkono uhusiano mwema kati ya Israel na Marekani, baada ya uhusiano kati ya pande mbili kuyumba wakati wa utawala wa Barack Obama.

Rais huyo wa zamani alikosoa vikali ujenzi wa makaazi ya Wayahudi katika eneo la Ukingo wa Magharibi yaliyoidhinishwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

Kwa miongo serikali za Marekani zimeunga mkono kuwepo kwa nchi huru ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa taifa huru la Palestina ambalo litakua jirani mwema na Israel.

hata hivyo hii ilionekana kubadilika hapo Jumanne baada ya afisa wa Ikulu kusema Marekani inaunga mkono mpango mbadala wa kuafikia amani na siyo tu kuwepo kwa nchi mbili huru.

Kuwepo kwa nchi mbili huru imeonekana kama njiya pekee ya kumaliza vita vya miongo mingi kati ya Israel na Palestina.

Ni msimamo unaoungwa mkono na jamii ya kimataifa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Makaazi ya Walowezi wa Kiyahudi katika arthi ya Palestina

Muafaka huu utawezesha kuundwa kwa taifa huru la Palestina ambalo mipaka yake itaambatana na mkataka wa mwaka 1967.

Taifa la Palestina litajumuisha Ukingo wa Magharibi, Ukanda wa Gaza, na Mashariki mwa Jerusalem, na litaweka amani kama jirani wa Israel.

Taarifa zinasema baadhi ya maafisa wa Israel wenye msimamo mkali wanamshinikiza Rais Trump kuachana na mpango wa nchi mbili huru.

Aidha wanaamini ardhi inayotakikana kwa taifa la Palestina ni eneo la Israel.

Zaidi ya Wayahudi 600,000 wanaishi katika makaazi 140 ambayo yamejengwa na Israel tangu mwaka wa 1967 katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi na Mashariki mwa Jerusalem.

Chini ya sheria ya kimataifa makaazi haya ni haramu, japo Israel inapinga hilo.