Gyan aonywa kuhusu mtindo wake wa nywele UAE

Mtindo wa nywele wa Asamoah Gyan hauna maadili mema lasema shirikisho la soka la UAEFA
Image caption Mtindo wa nywele wa Asamoah Gyan hauna maadili mema lasema shirikisho la soka la UAEFA

Aliyekuwa mshambuliaji wa klabu ya Sunderland nchini Uingereza Asamoah Gyan ni miongoni mwa kundi la wachezaji 40 wanaodaiwa kuwa na mtindo wa nywele ''usio na maadili mema'' chini ya maelezo ya shirikisho la soka la UAE.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 kutoka Ghana yuko kwa mkopo katika klabu ya Al Ahli katika ligi ya Dubai ya Arabian Gulf kutoka klabu ya Shanghai SIPG.

Baadhi ya mafunzo ya Kiislamu yanapinga mtindo wa nywele wa 'Qaza' ambapo ni eneo moja la nywele linalonyolewa.

Marefa huangalia iwapo nywele za wachezaji zimenyolewa vizuri.

Baadhi ya maafisa wanaosimamia mechi katika eneo la UAE hutilia mkazo sheria hizo kwa kuwa wana wasiwasi kwamba huenda watoto wao wakaiga mitindo hiyo.

Maelezo kama hayo yametolewa katika mataifa jirani.

Mwaka 2012 mlinda lango wa Saudia Waleed Abdullah alilazimishwa na refa kukata nywele zake kabla ya kuchezea timu yake ya Al Shabab.

Shirikisho la soka la UAEFA hutuma barua ya onyo kwa mchezaji aliyenyoa nywele hizo kwa mara ya kwanza huku adhabu ikiongezeka na kutozwa faini na kupigwa marufuku iwapo atakataa kutekeleza onyo hilo.

Gyan ni mmojawapo wa wachezaji 46 waliopatiwa barua hizo.