Kesi ya washukiwa wa ugaidi yaanza Rwanda

Washukiwa wa jamii ya Kiislamu wanaotuhumiwa kushirikiana na kundi la Islamic State
Image caption Washukiwa wa jamii ya Kiislamu wanaotuhumiwa kushirikiana na kundi la Islamic State

Kesi ya kwanza ya watu wanaotuhumiwa na ugaidi imeanza kusikilizwa nchini Rwanda ikiwahusisha watu zaidi ya 50.

Watuhumiwa kutoka jamii ya Waislam nchini Rwanda wameshtakiwa kwa makosa ya kushirikiana na makundi ya kigaidi yakiwemo kundi la Islamic State.

Kulinagana na mwandishi wetu Yves Bucyana kutoka Kigali watuhumiwa 51 wameletwa mahakamani wakiwa wamevikwa pingu chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Wengi wa vijana hao ambao nyusoni mwao walionekana wakakamavu huku baadhi wakionekana kupiga soga na jamaa zao waliofurika katika chumba cha mahakama.

Baada ya saa kadhaa za kusoma maelezo binafsi ya kila mtuhumiwa, mwendesha mashitaka ameomba kesi kuendelea faraghani kwa hoja ya kwamba hii ni kesi nzito na pengine inayoweza kuhatarisha usalama wa taifa ikiwa itasikilizwa hadharani.

Mawakili wa washitakiwa wamepinga hoja hiyo wakisema haina msingi wakati huu ambapo upelelezi dhidi ya wateja wao ulimalizika na kwamba kwa ngazi hii hakuna hofu yoyote ya kupoteza ushahidi ama kuhatarisha usalama wa taifa.

Aidha upande wa utetezi umeweka pingamizi za kwamba baadhi ya washukiwa hawajatimiza umri wa miaka 18 ambapo mahakama hio haina mamlaka ya kuendesha kesi dhidi yao.

Watu hao wamezuiliwa kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa.

Tangu lilipoanza kujitokeza watu 4 ,wote Waislamu waliuawa katika nyakati tofauti kwa kupigwa risasi na polisi huku duru kutoka kwa polisi zikisema kwamba walikuwa katika njama za kusajili vijana wa kujiunga na kundi la Islamic State.

Suala hili la makundi ya ugaidi nchini Rwanda lilipoanza kuzungumzwa lilishtua wengi ambapo serikali ilithibitisha kuwa lipo na kusisitiza kuwa hatua kali inazochukua zinalenga kulikomesha kabisa kuvuka mipaka.

Kesi hii imeahirishwa hadi tarehe 15 mwezi ujao.