Trump ashutumu vyombo vya habari ,FBI na NSA

Rais Donald Trump amevishtumu vyombo vya habari na mashirika ya ujasusi nchini humo Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Rais Donald Trump amevishtumu vyombo vya habari na mashirika ya ujasusi nchini humo

Rais wa Marekani Donald Trump ameshtumu idara za upelelezi nchini humo na vyombo vya habari baada ya ripoti mpya za mawasiliano kati ya wanachama wa serikali yake na Urusi.

Bwana Trump amevishutumu vitengo vya ujasusi nchini humo NSA na FBI kwa kutoa habari kinyume na sheria.

Baadhi ya vyombo vya habari vinasema kuwa wasaidizi wake walikuwa wakiwasiliana mara kwa mara na maafisa wa Urusi wakati wa kampeni za uchaguzi.

Maafisa wa ujasusi awali walisema kuwa wanaamini kwamba Urusi ilijaribu kushawishi matokeo ya uchaguzi huo kwa niaba ya Trump.

Moscow imekana madai hayo ,ikiyataja kuwa yasiokuwa na msingi wowote.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema siku ya Jumatano kwamba ripoti za mawasiliano na wasaidizi wa Trump hazina msingi wowote.

Haki miliki ya picha Getty Images/reuters/AP/EPA
Image caption Waliokuwa wassaidizi wa Trump Former Trump Michael Flynn, Carter Page na Paul Manafort wanachunguzwa kwa madai ya kuhusishwa na Urusi

Siku ya Alhamisi Rex Tillerson anatarajiwa kufanya mkutano wake wa kwanza kama waziri wa maswala ya kigeni na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov katika mkutano wa G20 unaofanyika mjini Bonn nchini Ujerumani.

Hatua hiyo inajiri baada ya mshauri wa mkuu wa maswala ya usalama wa rais Donald Trump Michael Flynn kujiuzulu kufuatia ripoti kwamba alijadili vikwazo vya Marekani kwa simu na mwanadiplomasia wa Urusi kabla ya Trump kuchukua mamlaka.

Viongozi wa Republican wamejiunga na wito wa kufanya uchunguzi kuhusu uhusiano wa Flynn na Urusi.