Waziri wa bajeti asema uchaguzi utagharimu dola bilioni 1.8

Wapinzani wa rais Kabila wamemshtumu kwa kuchelewesha uchaguzi Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wapinzani wa rais Kabila wamemshtumu kwa kuchelewesha uchaguzi

Umoja wa Mataifa ,Muungano wa bara Ulaya na Umoja wa Afrika zimeonyesha wasiwasi wao katika kile walichokitaja kuwa mzozo katika majadiliano ya kisiasa nchini DR Congo.

Hatua hiyo inajiri baada ya waziri wa bajeti nchini humo Pierre Kangudia kusema kuwa taifa hilo halitaweza kugharamia maandalizi ya uchaguzi wa urais mwaka huu.

Uchaguzi huo ni miongoni mwa makubaliano yalioafikiwa katika kumaliza mgogoro unaoendelea.

Taifa la Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo lilisema kuwa halitaweza kugharamia uchaguzi wa urais mwaka huu ,kulingana na serikali.

Waziri wa bajeti Pierre Kangudia alisema kuwa gharama ya kuandaa uchaguzi huo ambayo ni takriban dola bilioni 1.8 ni ghali mno.

Mwaka uliopita serikali na upinzani walikubaliana kwamba uchaguzi mpya utafanyika mwishoni mwa mwaka 2017.

Utawala wa rais Kabila ulikamilika mnamo mwezi Novemba 2016.

Wapinzani wa Kabila wamemshutumu kwa kuchelewesha uchaguzi ili kusalia madarakani.

Mpango wa kufanya uchaguzi kabla ya mwisho wa mwaka 2017 awali ulipunguza wasiwasi kati ya ya serikali na upinzani.

Tume ya uchaguzi ilisema mnamo mwezi Novemba kwamba ilihitaji hadi mwezi Julai 2017 kusajili zaidi ya wapiga kura milioni 30 katika taifa lililo na ukubwa sawa na Ulaya Magharibi, lakini likiwa na hali mbaya ya uchukuzi pamoja na mawasiliano duniani.

Mapema mwezi huu, kifo cha kiongozi wa upinzani Etienne Tshisekedi kilizua wasiwasi kuhusu hatma ya taifa hilo.

Uchaguzi nchini DR Congo hukabiliwa na migogoro kila wakati. Mwaka uliopita maandamano dhidi ya hatua ya kutaka kuchelewesha uchaguzi wa urais yalisababisha vifo vya takriban watu 50.

DR Congo haijawahi kuwa na uhamisho mzuri wa mamlaka tangu taifa hilo lijipatie uhuru zaidi ya miaka 55 iliopita.

Rais Kabila alichukua mamlaka mwaka 2001 kufuatia mauaji ya babake Laurent Kabila. Ameshinda uchaguzi mara mbili na katiba inamzuia kuwania kwa awamu ya tatu.