Msanii Roma Mkatoliki atoweka Tanzania

Msanii Roma Mkatoliki akamatwa Haki miliki ya picha Twitter
Image caption Msanii Roma Mkatoliki akamatwa

Msanii wa bongo Fleva kutoka Tanzania Ibrahim Musa aka Roma Mkatoliki ametoweka baada ya kudaiwa kukamatwa mapema siku ya Alhamisi katika mji wa Dar es Salaam.

Inadaiwa alichukuliwa katika studio moja katika mji huo pamoja na mtayarishaji wake.

Ripoti nyengine zinasema kuwa vifaa vyake vya kurekodi pia vilichukuliwa.

Raia wamekuwa wakisambaza habari katika mtandao wa Twitter:

Familia za wawili hao zinasema kuwa zimetembelea vituo vya polisi ,lakini hazijaweza kuwapata.

Joff Msumule, rafikiye mzalishaji huyo amesema kuwa maafisa wa polisi walikuwa wanatafuta ushahidi wa kuwashtaki wanamuziki hao.

Sikuwepo lakini naeleza kwamba kulikuwa na wimbo uliotayarishwa ambao inadaiwa hautoi ujumbe mzuri kwa serikali.

Haki miliki ya picha Twitter
Image caption Ujumbe uliosambazwa katika mtandao wa Twitter baada ya Roma Mkatoliki kukamatwa

Wimbo huo haukurekodiwa katika studio ya Tongo, lakini msanii alitumia chapa ya studio hio.

Hii inamaanisha kwamba sisi ndio tuliourekodi wimbo huo kwa hivyo maafisa wa polisi walikuja kuchukua ushahidi.

Joseph Mbilinyi msanii wa zamani ,ambaye kwa sasa ni mbunge aliwasilisha swala hilo bungeni kwa kudai kuwa serikali ilikuwa ikitumia majasusi wa siri kuwakamata raia.

Habari hiyo inajiri wiki kadhaa baada ya msanii mwengine wa Bongo Fleva Ney wa Mitego kukamatwa kwa wimbo uliodai kuwa serikali inakandamiza uhuru wa kujieleza, hatua ilioonekana kutusi serikali ya rais John Pombe Magufuli.

Baadaye aliwachiliwa huru kufuatia malalamishi ya umma lakini akaambiwa kuimarisha wimbo huo ili kujumuisha maswala mengine yanayoathiri Tanzania.